Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TFDA Yafuta Usajili wa Dawa Zenye Madhara kwa Binadamu
Nov 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Prisca Libaga-MAELEZO, Arusha.

Mamlaka ya chakula na dawa TFDA  imezifutia usajili dawa mbalimbali za kutibu magonjwa ya binadamu na kuziondoa  kwenye soko pamoja na kusitisha  matumizi yake  kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa wagonjwa.

Hayo yameelezwa jana Jijini Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw. Hiiti Sillo, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya wakufunzi  wa ufuatiliaji   juu ya ufundishaji na uhamasishaji  wa masuala ya udhibiti  wa madhara yatonayo na matumizi ya dawa zisizosalama kwa watendaji wa afya kutoka Wilaya zote za mkoa wa Arusha.

Bw. Sillo mesema katika kudhibiti matumizi ya dawa zisizofaa TFDA imeondoa  dawa ya sindano aina ya Chloramphenical  kwenye soko  baada ya shirika la afya Duniani WHO,  kubaini dawa hiyo ina  madhara  kwa watumiaji, Pia mamlaka hiyo imefuta usajili wa dawa  zingine kama vile Ketoconazole, (vidonge) Phenylpropanalamine,Dextropropoxyphene,Nimesulide,stavudine 40, Gatifloxacin,Rofecoxib, pamoja na Celecoxib baada ya kuthibitika zina madhara kwa watumiaji.

Aidha matumizi ya dawa kama vile Kanamycin,Amikacin na Levofloxacin  zimebadilishwa  ili ziweze kutumika  kwa ajili ya kutibu ugonjwa  wa kifua kikuu pekee.

Mkurugenzi huyo wa TFDA amesema mafunzo hayo yanashirikisha wakufunzi 60 nchini kote na yanafanyika katika mikoa mbalimbali  yakiwashirikisha Madaktari, Manesi, na wafamasia  walioko kwenye  hospitali, vituo vya afya na Zahanati.

Bw.Sillo alieleza kwamba, lengo la mafunzo hayo ni kuongeza idadi ya wakufunzi wa masuala ya usalama wa dawa  kutoka 73  hadi 133  na tayari katika kipindi cha miaka mitatu 2014/ 15 hadi 2017/18, Mamlaka ya chakula na dawa imehamasisha watendaji wa afya wapatao 2000 nchini kote na sasa uhamasishaji unaendelea  katika mkoa wa Katavi.

Alisema mara baada ya mafunzo hayo wakufunzi hao  watafundisha wenzao  kwenye maeneo yao ya kazi  ili kuongeza uelewa kwa wataalam wengi zaidi  kufahamu  taratibu zilizoko  za udhibiti wa madhara  yanayotokana na matumizi ya dawa zisizofaa.

Aliwakumbusha wakufunzi hao kwamba  kila mtendaji wa afya  ana wajibu wa  kulinda afya za wagonjwa anao watibu au kuwahudumia  na wajibu huo  ni pamoja na kuhakikisha wagonjwa wanabaki salama  na ikiwa watapata madhara  hatua za kuwatibu zinachukuliwa  na kutoa taarifa ili kuzuia kusambazwa zaidi kwa dawa zinazoleta madhara.

Bw. Sillo alifafanua kuwa, kumekuwa na baadhi ya wataalam wa afya  kudhani kuwa  kwa kutoa taarifa kuwa dawa ina madhara inaonekana kuwa wao ndio wanaosababisha madhara hayo na kusisitiza kuwa dhana hiyo sio ya kweli, hivyo  akawasisitiza watoe taarifa  sahihi  ili wananchi wafahamu madhara yatokanayo na matumizi ya dawa pamoja na hatua za kuchukua.

Mamlaka ya chakula na dawa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma  wametengeneza mfumo wa kielektroniki  wa utoaji wa taarifa za usalama  na madhara ya dawa  ambao ulizinduliwa Oktoba 2016  na Waziri wa afya Mh.Ummy Mwalimu.

Kabla ya kuzinduliwa mfumo huo taarifa za usalama na madhara ya dawa  zilikuwa zikitolewa kwa kutumia fomu maalumu za njano ,kijani na blue  ambapo watoa huduma za afya walikuwa wakitumia fomu za njano huku wagonjwa wakitoa taarifa kwa kutumia fomu za  za kijani, na fomu za bluu zilitumika kutoa taarifa  za ubora wa dawa na kama kuna dawa duni au bandia kwenye soko.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi