Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TFDA Kielelezo cha Huduma Bora Kimataifa
Jun 14, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Frank Mvungi

Maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA ) imekuwa kielelezo  cha utoaji wa huduma bora na  kukidhi viwango vya kimataifa, hivyo kuifanya  kuwa moja ya maabara zinazotambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ubora ambapo majibu yanayotolewa katika maabara hii yanatambulika kimataifa.

Ni katika utendaji huo, maabara ya uchunguzi wa chakula na  ya maikrobaiolojia zimepata ithibati kwa kiwango cha Kimataifa ISO/IEC 17025:2005 baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa.

Tuna kila sababu ya kujivunia taasisi hiyo kwa kuwa imekuwa mfano mzuri kwa utendaji barani Afrika kutokana na kutekelezwa kwa mfumo wa utoaji huduma (QMS) sanjari na mifumo ya kielektroniki Taasisi hiyo imefanikiwa kushika nafasi ya pili na kuwa ya mfano kwa uongozi na utendaji (Best Managed Institution) kati ya wizara,idara,taasisi na wakala zote za Serikali kwa mwaka 2010 ,2011, na  2015

Siwapongezi TFDA kwa hayo tu bali kwa hili la kutambua changamoto zinazowakabili wajasiriamali  katika usajili wa majengo na bidhaa zao.Kuwepo kwa mkataba wa maridhiano (MOU) na Shirika la Viwango Tanzania  ni kichocheo cha kukuza sekta ya Viwanda hasa kipindi hiki tunapojenga uchumi wa viwanda, mkataba huu unatambua mchango wa kila taasisi katika tasnia ya ujasiriamali wa bidhaa zinazodhibitiwa na mamlaka na namna ya kupunguza gharama ya usajili.

Aidha, TFDA itatumia matokeo ya TBS ya vipimo vya maabara kusajili bidhaa husika ambapo TBS itazingatia usajili wa TFDA wa majengo na bidhaa wakati wa kutoa alama ya ubora.

Dhamira ya TFDA ni kutoa mafunzo kwa wasindikaji ili kuwajengea uwezo katika masuala yanayohusu usindikaji vyakula ambapo wajasiriamali takribani 2000 wameshapatiwa mafunzo hayo tangu kuanzishwa kwa progamu hii. Jambo hili ni ishara njema hasa wakati huu ambapo Serikali inasisitiza ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Tumekuwa tukishuhudia wataalamu kutoka Mamlaka za udhibiti wa Bidhaa za chakula kutoka katika nchi za Zambia, Botswana,Msumbiji,Burundi, Nigeria, Ghana,Cameroon,Ghana,Kenya,Ethiopia,Liberia,Rwanda,Sudan, ya kusini, na Uganda lengo likiwa kujifunza jinsi mamlaka yetu ilivyofanikiwa.

Jambo jingine la kujivunia ni kuwa, TFDA imeteuliwa kuwa taasisi kiongozi katika kuandaa miongozo ya uwiano wa usajili wa dawa miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hii ni pamoja na utekelezaji wa  mpango wa miaka mitano (2012-2016) wa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa dawa.

Pia Mamlaka hiyo imefanikiwa kupewa zabuni za Kimataifa katika uchunguzi wa kimaabara kutoka nchi mbalimbali kama vile Rwanda na Liberia, huu ni ushahidi kuwa Tanzania imepiga hatua katika kutoa huduma bora.

Ongezeko wa wateja wanaoridhika na huduma kwa wateja wa ndani na nje ya nchi kwa mujibu wa utafiti  uliofanywa mwaka 2013/2014 ni ishara tosha kuwa mamlaka hii imepiga hatua kubwa kimataifa.Kiwango cha kuridhika kwa wateja wa ndani na nje kimefikia asilimia 74.4 na 67 ukilinganisha na asilimia 63 na 66 mwaka 2008.

Katika kuhakikisha kuwa TFDA  inaendelea kuwa juu kimataifa,imejipanga kuendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda afya ya jamii kwa kuimarisha na kubuni mbinu mbadala za udhibiti kwa kuzingatia sheria,maendeleo ya kisayansi,kiteknolojia na mawasiliano pamoja na kushirikisha wadau.

TFDA ilianzishwa chini ya Sheria ya Chakula,Dawa na Vipodozi sura ya 219, kwa lengo la kulinda afya ya watumiaji vyakula,dawa,vipodozi, na vifaa tiba,hii inamaanisha kuwa wanaolindwa ni sisi sote ikiwa ni pamoja na sisi tuliopo hapa ,jamaa zetu na wananchi kwa ujumla.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi