Mkufunzi Mkazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Dodoma Bw. Habibu Muyula akisisitiza kuhusu umuhimu wa mafunzo kwa wasichana waliokosa elimu katika mfumo rasmi kutokana na kupata ujauzito wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma kukagua maendeleo ya wahitimu wa mafunzo hayo kwa awamu ya kwanza ambao ni matokeo ya mradi wa kuzuia mimba za utotoni unatekelezwa na Taasisi hiyo na washirika wa maendeleo.
Na Frank Mvungi
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) yaendelea Kuwawezesha Wasichana waolikosa elimu katika mfumo rasmi na wale waliopata ujauzito katika Wilaya ya Bahi na Kongwa Mkoani Dodoma.
Akizungumza wakati wa mahojiano maalum kuhusu kukamilika kwa mafunzo ya awamu ya kwanza kwa wasichana hao Mkufunzi Mkazi wa Taasisi hiyo Mkoa wa Dodoma Bw. Habibu Muyula amesema kuwa mradi huo wa kuzuia mimba za utotoni umepata mafanikio makubwa ambapo wahitimu wake wamejifunza kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo batiki, sabuni na unga wa lishe.
Katika mafunzo hayo wahitimu hao wameweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo stadi za maisha kama vile uraia, elimu ya uraia,mazingira, kujitambua na elimu ya afya.
"Katika mafunzo waliyopata wahitmu hawa wa awamu ya kwanza takribani 159 katika Wilaya ya Bahi sasa wameanza kuzalisha bidhaa mbalimbali hali itakayosaidia kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika kujenga uchumi wa viwanda " Alisisitiza Muyula
Akifafanua Muyula amesema kuwa wahitimu wa mafunzo hayo wanapaswa kutumia fursa ya Dodoma kuwa jiji kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuendana na mahitaji ya soko ili waweze kushiriki Kikamilifu katika kuleta maendeleo.
Pia alitoa rai kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwaruhusu wasichana waliokosa elimu katika mfumo rasmi kutokana na mimba za utotoni na sababu mbalimbali kutumia fursa ya kuwepo kwa mradi huo kupata mafunzo kwa kujitokeza na kujiandikisha ili awamu ya pili ya mradi iweze kuanza.
Kwa upande wake Mmoja wa Walimu wa Mafunzo hayo Bw. Richard Chuma amesema kuwa washiriki wa mafunzo hayo walikuwa na mwamko mkubwa hali iliyochochea kufanikiwa kwa mafunzo hayo.
Aidha alitoa wito kwa wazazi na Jamii kwa ujumla kuwarusu wasichana waliokosa elimu katika mfumo rasmi kutokana na mimba za utotoni na sababu mbalimbali kuwasaidia ili waweze kushiriki katika mafunzo hayo ya awamu ya pili inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo awamu ya kwanza Bi Sophia Kassim amesema kuwa baada ya mafunzo hayo wamepata mabadiliko makubwa na sasa wanajitambua hali inayowawezesha kushiriki katika kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo batiki, sabuni na unga wa lishe.
Pia alitoa wito kwa wasichana waliokosa elimu katika mfumo rasmi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba kujitokeza kushiriki katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wasichana hao awamu ya pili itakayoanza hivi karibuni katika Wilaya ya Bahi na Kongwa Mkoani Dodoma unakotekelezwa mradi huo.
Mradi wa kuzuia mimba za utotoni unatekelezwa katika Wilaya ya Bahi na Kongwa Mkoani Dodoma na umeonesha mafanikio makubwa kwa awamu ya kwanza ambapo washiriki zaidi ya 348 wameshanufaika na mradi huo.