Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameitaka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kuhakikisha inatelekeza ipasavyo Mradi wa Kuinua Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa kuwa TEWW moja ya Taasisi inayotekeleza mradi huo.
Waziri Ndalichako ametoa maagizo hayo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Wajumbe wa Baraza la Usimamizi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.
Amesema ni vizuri mradi huo ukatekelezwa ipasavyo ili malengo ya mradi yaweze kufikiwa ambapo moja kati ya malengo hayo ni kuwezesha mtoto wa kitanzania kuendelea kupata elimu bora.
Aidha, Prof. Ndalichako amesisitiza TEWW kuendelea kufanya kazi ninazoendana na dhima wa uanzishwaji wa Taasisi hiyo ikiwepo utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa ya Kisomo maarufu kama ‘NALMES’ pamoja na kuandika maandiko kwa ajili ya miradi mingine kwa ajili ya kuwawezesha watanzania.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndalichako amepongeza Baraza la Usimamizi wa TEWW kwa kufanya majukumu yake kwa ufanisi mkubwa toka ilivyozinduliwa mnamo Agosti, 2018.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Dkt. Michael Ng’umbi amemwakikishia Waziri kuwa TEWW itatekeleza mkakati wa Kisomo wa Kitaifa (NALMES) na ule wa SEQUIP kama ambavyo ilivyokusudiwa kwa ajili ya maslahi mapana ya Tanzania.