Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBS Yatoa Elimu ya Sumukuvu katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,Tanga
Dec 18, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu ya sumukuvu katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga ili wananchi wapate uelewa wa sumukuvu, madhara yake na jinsi ya kuidhibiti.

Elimu hii iliyotolewa na TBS kupitia radio za kijamii zilizopo mikoani humo iliwahusisha pia wizara ya kilimo. Mtaalam kutoka TBS Dkt. Analice Kamala akitoa elimu hiyo alisema kuwa sumukuvu ni sumu inayozalishwa na jamii ya fangasi wanapoingia kwenye mazao ya chakula yakiwa shambani, wakati wa kusafirisha au wakati wa kuhifadhi.

"Sumukuvu haionekani kwa macho, haina ladha wala rangi na pia inapoingia kwenye chakula haiondolewa kwa njia za kawaida za kupika au kusindika chakula. Alisema kuwa uwepo wa sumukuvu kwenye mazao ya chakula hutegemea hali ya hewa (joto na unyevu) ya enao mazao yanapolimwa na kiasi cha unyevu kwenye mazao.

Dkt. Kamala alisema uchafuzi wa sumukuvu unatofautiana kulingana na aina ya mazao ingawa mazao ya mahindi na karanga ndiyo huathirika zaidi.

Dkt. Analice Kamala alisema sumukuvu humfikia mlaji kupitia ulaji wa mazao ya chakula yaliyochafuliwa na sumukuvu hususan mahindi na karanga, mazao ya mifugo ambayo imelishwa chakula kilichochafuliwa na sumukuvu kama vile maini na maziwa.

Vilevile alisema mtoto anayenyonya huweza kupata sumukuvu kama mama anayenyonyesha atakula chakula kilichochafuliwa na sumu hizo. Dkt. Kamala alisema wakulima wanapaswa kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usafi wa shamba, kutumia mbegu zilizodhibitishwa na wataalam, kupanda kwa wakati, kuwa na mzunguko wa mazao kwa kubadilisha mazao ya kilimo, kuvuna kwa wakati, kuepuka kulundika mazao shambani, kusafirisha kwa kutumia vifaa ambavyo ni vikavu, kutokuanika kwenye udongo.

Dkt Kamala aliongeza kuwa mazao ya chakula hususan mahindi na karanga yaliyooza au yenye ukungu yanatakiwa kuchambuliwa na kuondolewa kwani yana kiwango kikubwa cha sumukuvu, hivyo yakiliwa na binadamu au wanyama huweza kusababisha madhara" alisema.

Akizungumzia madhara ya sumukuvu Mtaalam Dkt. Candida Philip alisema sumukuvu hususan aina ya aflatoxin inapoingia mwilini inasababisha madhara ya kiafya na hujitokeza baada ya muda mfupi au mrefu kutegemea kiasi cha sumukuvu katika chakula, chakula chenye sumukuvu kimeliwa kwa wingi kiasi gani, umri wa mlaji na hali ya kiafya kwa ujumla.

Dkt. Candida Philip alisema kuwa chakula kilichochafuliwa na sumukuvu kwa kiwango kikubwa sana husababisha madhara ya moja kwa moja kwenye ini na dalili zake ni tumbo kuuma, kutapika, kuharisha, tumbo kuvimba, rangi ya njano kwenye macho, viganja na nyayo, degedege hadi kifo.

Alisema ikiwa kiwango cha sumukuvu aina ya aflatoxin kimeliwa kwa kiwango kidogo lakini kwa kipindi cha muda mrefu kuna uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya ini na hii imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani.

Madhara mengine yanayoweza kujitokeza baada ya muda mrefu ni pamoja na udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano na kuathirika kwa kinga mwili. Mbali na athari za kiafya, pia kiuchumi sumukuvu huathiri nguvu kazi, huongeza gharama za matibabu, biashara na uhakika wa chakula.

Elimu hii iliyotolewa kupitia radio za kijamii za Arusha FM na Safina FM (mkoani Arusha), Moshi FM na Kicheko FM (mkoani Kilimanjaro), TK FM na Mwambao FM (mkoani Tanga) na imewafikia wakazi wa mikoa husika na mikoa ya jirani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi