Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBS Yatoa Elimu Madhara ya Sumukuvu
Jul 30, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na Neema Mtemvu - TBS

Wananchi  wa Handeni wakipata elimu wakipata kuhusiana na sumukuvu

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu kuhusiana na sumukuvu, madhara yake na jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo ili kujenga uelewa kwa wananchi wa Wilaya za Handeni na Kilindi mkoani Tanga.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa utoaji elimu hiyo, Afisa Usalama wa Chakula Mkuu wa TBS, Dkt. Candida Shirima alisema elimu hiyo imetolewa kwenye wilaya hizo kwa kuwa zipo kwenye ukanda wenye hali ya hewa inayowezesha ustawi wa fangasi wanaozalisha sumukuvu kwenye mazao ya chakula.

"TBS imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la sumukuvu kwa lengo la kulinda afya ya jamii na kuwezesha biashara ya mazao ya chakula", alisema Dkt. Shirima.

Aliongeza kuwa TBS imechukua hatua hiyo muhimu ya kutoa kipaumbele katika kuelimisha jamii namna ya kukabiliana na sumukuvu hususan katika kipindi hiki cha msimu wa mavuno ya mahindi.

Vile vile elimu imetolewa ili wananchi waweze kufahamu taratibu muhimu zinazopaswa kuzingatiwa ili kukabiliana na sumukuvu katika mnyororo wa mazao kuanzia yanapokuwa shambani na baada ya kuvunwa wakati wa kukausha, usafirishaji, uhifadhi na uandaaji.

Kwa mujibu wa Dkt. Shirima, sumukuvu (mycotoxins) ni sumu zinazozalishwa na jamii ya fangasi kwenye mazao ya chakula na kwamba mazao yanayoathiriwa zaidi ni nafaka hasa mahindi na mbegu za mafuta zikiwemo karanga.

Alieleza kuwa mambo yanayowezesha uzalishaji wa sumukuvu ni pamoja na uwepo wa jamii ya fangasi husika na kuchochewa na hali ya hewa ya joto kali na unyevu, ukame na wadudu waharibifu.

Kupitia elimu liyotolewa, jamii ilielimishwa pia kuhusu madhara ya kiafya yatokanayo na sumukuvu ambayo huweza kujitokeza ndani ya muda mfupi ikiwa ni pamoja na maumivu ya tumbo, kuathirika kwa ini na hata kifo endapo mtu atakula kiwango kikubwa sana cha sumukuvu ambacho mwili hautaweza kukihimili.

Aidha, sumukuvu huweza pia kusababisha madhara yanatokea baada ya muda mrefu ambayo ni pamoja na saratani ya ini, upungufu wa kinga mwili na udumavu.

Kuhusu namna ya kudhibiti sumukuvu kwenye mazao, Dkt. Shirima alihimiza hatua muhimu zichukuliwe kabla na baada ya kuvuna mazao ikiwemo ya kupanda kwa wakati mbegu zilizothibitishwa na taasisi za udhibiti wa viwango vya ubora wa mbegu, kuhakikisha shamba ni safi wakati wote, kutumia viuatilifu mara wanapoona dalili za wadudu au magonjwa kwenye mazao, kuvuna kwa wakati na kuondoa mazao shambani mara baada ya kuvuna.

Aliwaambia walengwa wa elimu hiyo kwamba kuchelewa kuvuna au kulundika mazao muda mrefu shambani huchochea uzalishaji wa sumukuvu.

Kuhusu udhibiti wa sumukuvu kwenye mazao baada ya kuvuna, Dkt. Shirima aliwaambia walengwa wa elimu hiyo kuwa baada ya kutoa mazao shambani, taratibu nyingine zote zinazofuata zifanyike kwa umakini ili kuzuia mazao kupata mashambulizi ya fangasi wanaozalisha sumukuvu.

"Ni muhimu kuhifadhi mazao kwenye ghala au chumba kisafi, kinachoruhusu mzunguko wa hewa, kutumia vifaa vyenye ubora kama vile magunia, mifuko au mapipa kuhifadhia mazao na kuepuka kuchanganya mazao ya zamani na mazao mapya", aliongeza Dkt. Shirima.

Wakizungumzia kuhusu elimu iliyotolewa, baadhi ya wananchi wa Wilaya hizo waliishukuru Serikali kwa jitihada zinazofanyika ili kuhakikisha usalama wa chakula na kuahidi kutekeleza yote waliyofundishwa na kuwa mabalozi kwa wananchi na wakulima ambao hawatakuwa wamepata elimu hiyo.

Nao wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliopata elimu hiyo walisema wataifikisha kwa wazazi wao na watasimama imara kuhakikisha mazao ndani ya familia zao hayashambuliwi na sumukuvu.

Wataalam wa TBS wametoa elimu ya sumukuvu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na wananchi wengine kwa ujumla katika wilaya hizo kupitia kwenye shule, masoko, minada, mikutano ya vijiji, magulio, kliniki za mama na mtoto na maeneo mengine ya biashara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi