Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBS Yatoa Elimu kwa Waagizaji wa Bidhaa na Mawakala wa Forodha
Sep 13, 2019
Na Msemaji Mkuu

                               Na Mwandishi Wetu

WAAGIZAJI wa bidhaa na mawakala wa forodha nchini, wamepatiwa elimu kuhusiana na taratibu za uingizaji wa bidhaa nchini pamoja na usajili wa maghala ya kuhifadhi bidhaa za chakula na vipodozi.

Maeneo mengine ambayo wamepatia elimu ni kuhusu taratibu za kufanya maombi kwa njia ya mtandao (OAS) pamoja na kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo, hususan kwenye masuala ya viwango na mifumo ya udhibiti ubora.

Wadau hao walipatiwa elimu hiyo jijini Dar es Salaam jana kupitia semina waliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Akifungua semina hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya, Mkurugenzi Upimaji na Ugezi wa shirika hilo, Johannes Maganga, alisema semina hiyo imewashirikisha washiriki mbalimbali ikiwemo wa kutoka Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Baraza la Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).

Wengine ni wawakilishi kutoka Shirikisho la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) na wadau wengine.

Alisema lengo la elimu hiyo ni kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zenye tija kwa taifa bila kuathiri taratibu na sheria za nchi. Kutokana na umuhimu huo, alisema ndiyo maana semina hiyo imewalenga waagizaji wa bidhaa mbalimbali na mawakala wa forodha nchini.

Maganga alisema, ili kutimiza majukumu ya shirika hilo ni muhimu kwa umma wa Watanzania kwenda sambamba na mikakati mingine ya kitaifa. Alifafanua kwamba shirika hilo limeendelea kutoa semina kama hizo kwa waagizaji wa bidhaa mbalimbali zitokazo nje na mawakala wa forodha katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tanga.

"Lakini tumepanga kufanya semina kama hii katika Mkoa wa Mbeya hivi karibuni," alisema. Alifafanua kwamba kwa kuzingatia kifungu cha 36 cha sheria ya viwango Na: 2 ya mwaka 2009, Serikali ilipitisha kanuni ya udhibiti wa shehena kupitia notisi ya Serikali Na: 405 ya Desemba 25, 2009.

Alisema kanuni hizo ziliipa TBS mamlaka ya kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingia nchini kabla ya kusambazwa kwenye soko la ndani.

Kwa mujibu wa Maganga, Februari Mosi 2012 ndipo shirika lilianzisha mfumo wa ukaguzi wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja nchini (PVoC) kama mpango wa kudhibiti ubora wa bidhaa katika nchi zinakotoka, ambao unasaidia kutatua changamoto zinazokuwepo wakati bidhaa zinapokuwa zinakaguliwa baada ya kufika nchini.

Alitaja changamoto hizo kuwa ni mabadiliko ya mifumo ya uondoshaji wa shehena bandarini kwa kutumia mfumo wa kielektroni, hasara ambazo wafanyabiashara walikuwa wanapata kutokana na kuharibiwa kwa bidhaa zinazopatikana kutokidhi viwango, hasara kwa Serikali kupitia matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa hizo na athari kwa mazingira wakati wa uteketezaji wa bidhaa zilizofeli vipimo.

Akitoa mada kwenye semina hiyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Bidhaa baada ya kuwasili nchini, Athuman Kissumo aliwaeleza washiriki kuhusiana na faida za uamuzi wa Serikali kurejesha TBS majukumu yaliyokuwa yakisimamiwa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Hiyo ni kutokana na mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2019 ambayo yameleta mabadiliko katika sheria ya viwango Na: 2 ya mwaka 2009, ambapo majukumu ya kudhibiti ubora na usalama wa chakula na vipodozi yanafanywa na shirika hilo.

Alitaja huduma zinazotolewa na shirika hilo kwa sasa kuwa ni usajili wa jengo, kusimamia masuala ya usalama na ubora wa chakula na vipondozi na upimaji wa bidhaa za vyakula na vipodozi kwa lengo la kudhibiti ubora.

Majukumu mengine ni utoaji wa leseni au cheti cha TBS kwa bidhaa za chakula na vipodozi na usajili wa bidhaa za vyakula na vipodozi vinavyotoka nje ya nchi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi