Na Mwandishi Wetu Shirika la ViwangoTanzania (TBS) limetumia Wiki ya Uwekezaji mkoani Kagera kutoa elimu ya viwango kwa wajasiriamali na umuhimu wa kupata alama ya ubora ambayo inatolewa bure.
Akizungumza na washiriki wa maadhimisho ya Wiki ya Uwekezaji iliyoanza Agosti 12 ikitarajia kumalizika kesho (Agosti 17) Afisa Uhusiano Neema Mtemvu, alisema gharama za wajasiriamali kupata alama za ubora ni bure, kwani zinalipwa na Serikali.
Alisema wajasiriamali wakishapata barua ya utambulisho kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na kuipeleka TBS, mchakato wa kuwapatia alama ya ubora unaanza mara moja.
"TBS inatambua mchango wa wajasiriamali katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi wengi, ndiyo maana tuna mchakato endelevu wa kutoa elimu kwa wajasiriamali kwa kuwa na hilo ni sehemu ya majukumu yetu ili waweze kupata alama ya ubora," alisema Mtemvu.Alisema katika kuelekea uchumi wa viwanda ni lazima kuzingatia viwango, ndiyo maana wamekuwa wakishiriki maonesho mbalimbali ikiwemo wiki ya uwekezaji mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa elimu.
Mtemvu alitoa wito kwa wajasiriamali akisema suala la wao kukidhi matakwa ya viwango vya kitaifa kwa bidhaa wanazozalisha na zinazosindikwa ni la msingi kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi.
Hii ni fursa muhimu ambayo inamlenga kumwinua mzalishaji aweza kushindana na kuuza bidhaa zake bila woga," alisisitiza.
Pia, Mtemvu alisema katika wiki ya uwekezaji wamepata fursa kuwapa taarifa washiriki kuwa baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakitekelezwa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ya chakula na vipodozi sasa hivi yamehamia TBS.
"Serikali ya Awamu ya Tano imeliona hilo na kwa hatua hiyo sasa inakuwa ni rahisi mno kupata alama ya ubora, kwani ukishapata alama ya ubora utaweza kufanya biashara na vile vile ule mzunguko uliokuwepo awali wa kuzunguka wa kwenda TFDA halafu urudi TBS utakuwa umepungua," alisema Mtemvu na kuongeza kwamba;
"Tunawasisitiza wajasiriamali na wafanyabishara wa mkoa wa kufika ofisi za shirika hizo kupata alama ya ubora." Alitoa mwito kwa Wakazi wa Kagera kuhakikisha wanatumia bidhaa zenye ubora, hasa kwa kuzingatia mkoa huo unapakana na nchi jirani, hivyo bidhaa nyingi zinaingia.