[caption id="attachment_17071" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza alipokuwa akifungua kikao kazi cha wataalam toka Taasisi za Udhibiti wa Dawa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) leo jijini Dar es Salaam.[/caption]
Na: Mwandishi Wetu
Tanzania imetoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutunga sheria zinazolingana ili kuwezesha udhibiti wa pamoja wa dawa na vifaa tiba zinazoingia katika nchi wanachama.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mpoki Dk. Ulisubisya Mpoki ametoa wito huo leo wakati akifungua Kikao cha Siku Mbili cha Kamati ya Maandalizi ya Mpango Ulinganishaji wa Kanuni za Usimamizi wa Dawa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika katika Hoteli ya New Africa jijiji Dar es Salaam.
“Juhudi za kweli hazina budi kuchukuliwa kudhibiti utengenezaji na uingizaji wa dawa zisizokidhi viwango ambazo mwishowe huwafikia watumiaji na matokeo yake ni wananchi kuathirika kwa kupata madhara makubwa kiafya”Dk. Mpoki alieleza
[caption id="attachment_17083" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha wataalam toka Taasisi za Udhibiti wa Dawa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki leo jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu)[/caption] Alisisitiza kuwa “magonjwa hayajui mpaka” hivyo uwepo wa dawa zenye ubora unaofanana katika nchi wanachama kunarahisisha matibabu kwa wagonjwa na kunaepusha matumizi ya dawa hafifu katika nchi moja ambako kunakoweza kusababisha usugu wa vidudu vya maradhi. Dk. Mpoki alieleza wajumbe wa Kamati hiyo ambao ni wawakilishi wa mamlaka za udhibiti wa dawa za nchi wanachama kuwa jukumu na wajibu wa kuhifadhi na kuinua afya ya jamii katika jumuiya lazima zitambuliwe na ziungwe mkono na nchi wanachama kupitia wizara zinazosimamia sekta ya afya. “Mamlaka hizi zimekuwa kama mlango unaolinda mfumo wa utoaji huduma za afya dhidi ya vifaa tiba na dawa zenye viwango duni, zisizo salama na zisizofanyakazi vyema kuingia katika masoko yetu“Dk. Mpoki alieleza. Alibainisha kuwa Tanzania ndio iliyopewa jukumu la kusimamia suala la kanuni hivyo kupitia ufadhili wa washirika mbali mbali wa maendeleo, watalaamu wanaohusika na usalama na dawa na vifaa tiba hukutana mara kwa mara kufanya tathmini kuangalia hatua iliyofikiwa. “Lengo la Jumuiya ni kuhakikisha kuwa ikifika mwisho wa mwaka huu dawa au kifaa tiba kikiingia katika moja katika nchi zetu kinakuwa na ubora ulio sawa” Dk. Mpoki. Katibu Mkuu huyo alieleza pia maazimio ya mkutano huo yatapelekwa, kupitia kwa makatibu wakuu, kwenye Kikao cha Mawaziri wa sekta husika kitakachofanyika nchini Uganda tarehe 23-25 Oktoba mwaka huu. Mkutano huu ulitanguliwa na mafunzo ya wiki mbili kwa wataalamu wa udhibiti na ukaguzi wa dawa kutoka nchi wanachama ambayo yalikuwa yakiendeshwa kwa pamoja kati ya TFDA na Shule ya Famasi ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi ya Afya Muhimbili. Akimkaribisha, Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) Bwana Hiiti Sillo aliwashukuru washirika mbalimbali wa Maendeleo ambao wamekuwa wakisaidia programu hiyo ya ulinganishaji kanuni za udhibiti na ukaguzi wa dawa.