Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa mradi wa miundombinu jumuishi ya uchukuzi, unaolenga kuunganisha bandari, reli, barabara na usafiri majini kupitia Ziwa Tanganyika ili kurahisisha na kupunguza muda wa usafirishaji wa mizigo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema hayo Agosti 18, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mapokezi ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Félix Tshisekedi, yaliyofanyika Ikulu Ndogo, Zanzibar.

Rais Samia amesema utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuchochea shughuli za kiuchumi kati ya Tanzania na Congo, sambamba na kuimarisha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Amesema katika mazungumzo yao, viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha biashara kwa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima, kuboresha huduma katika mipaka na kuwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika fursa za uwekezaji na biashara zinazojitokeza.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tunashirikiana na Congo katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, uchukuzi na miundombinu. Takwimu mpaka mwaka jana zinaonesha kwamba nchi yetu imefanya biashara ya takribani Shilingi bilioni 794,” amesema Rais Samia.

Sambamba na masuala ya uchumi na biashara, Marais hao wamejadili masuala ya amani na usalama, wakisisitiza kuwa utulivu ni nguzo muhimu katika kukuza maendeleo ya nchi, kanda na dunia kwa ujumla.
Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Félix Tshisekedi, amesema viongozi hao wameazimia kuendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo katika nyanja za uchumi, amani na utulivu, pamoja na afya.
Akizungumzia suala la mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Congo, Mhe. Tshisekedi amewataka Watanzania kutokuwa na hofu, akieleza kuwa nchi hiyo ina uzoefu na hatua zinazochukuliwa katika kudhibiti ugonjwa huo.
“Kuhusu suala la janga la Ebola nchini Congo, nawahakikishia Watanzania kuwa msiogope kuhusu hilo. Tunajua kinachotokea na tuna uzoefu wa jinsi ya kudhibiti,” amesema Mhe. Tshisekedi.

Aidha, Mhe. Tshisekedi amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutumia rasilimali zilizopo ndani ya bara hilo katika kutekeleza miradi ya maendeleo, badala ya kutegemea zaidi rasilimali kutoka nje ya bara.
“Tuna vitu vyetu wenyewe, tuna rasilimali za kutosha ikiwemo watu, madini na mengine mengi. Tukiboresha miundombinu ya barabara, bandari na nishati tutaweza kufanikisha suala hili,” amesema Mhe. Tshisekedi.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo, kupanua fursa za biashara na uwekezaji, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Tanzania, Congo na ukanda mpana wa Afrika Mashariki na Kati.