Tanzania imejipanga kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini kwenye sekta za kipaumbele ikiwemo; afya, nishati, madini, utalii, kilimo, uchumi wa buluu, sanaa na utamaduni katika maonesho ya Expo 2025 Osaka yatakayofanyika kuanzia tarehe 13 Aprili mpaka 13 Oktoba, 2025 Osaka nchini Japan.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade), Bi. Latifa M. Khamis ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 13, 2025 katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Amesema kuwa, faida zitakazopatikana kwa nchi ya Tanzania kushiriki katika maonesho ya Expo 2020 ni pamoja na kufungua fursa za biashara na masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini, kuvutia wageni watalii Tanzania pamoja na kutangaza miradi ya maendeleo inayohitaji mitaji, wabia na wawekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Vilevile, nchi itafaidika na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine zinazoshiriki, kutoa fursa kwa makampuni kujitangaza na kunadi bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini pamoja na kutangaza Kiswahili, mila, utamaduni na desturi za Watanzania.
"Ushiriki wa Tanzania umejikita katika kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini kwenye sekta za kipaumbele pamoja na juhudi za Serikali za kuwezesha uwekezaji na biashara ikiwemo miradi ya kimkakati ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege na nishati ya umeme na gesi", amesema Bi. Latifa.
Amefafanua kuwa, TanTrade inaendelea na uratibu wa ushiriki wa nchi kwenye maonesho hayo ambapo jumla ya programu 8 zimeandaliwa kwa makundi mbalimbali yatakayoshiriki ambazo ni; utalii ambayo itafanyika tarehe 25 Aprili hadi 6 Mei, 2025 na miundombinu tarehe 15 hadi 26 Mei, 2025.
Programu zingine ni kilimo, mifugo uvuvi na uchumi wa buluu tarehe 5 hadi 16 Juni, 2025; afya tarehe 20 Juni hadi 1 Julai, 2025; lugha ya Kiswahili na utamaduni tarehe 1 hadi 7 Julai, 2025; uwezeshaji wanawake tarehe 1 hadi 12 Agosti, 2025, nishati tarehe 17 hadi 28 Septemba, 2025 na sayansi na teknolojia tarehe 2 hadi 12 Oktoba, 2025.