Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaboresha Upatikanaji wa Haki Nchini
Jan 13, 2026
Na Timothy Mwakyenda - MAELEZO.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imeboresha huduma zake za utoaji wa haki kwa kuwafikia wananchi kwa ukaribu na kuongeza kasi ya utatuzi wa mashauri tofauti na kipindi cha nyuma ambapo mwananchi alikuwa anakaa muda mrefu kusubiri shauri  lake lisikilizwe.

Mhe. Masaju amesema  Serikali imesogeza huduma za kimahakama karibu na wananchi kwa kujenga Mahakama za wilaya kila wilaya Nchi nzima na kuendelea kukamilisha ujenzi kwa sehemu chache zilizobaki zikiwemo Mahakama za hakimu mkazi kila mkoa ili kuwasogezea wananchi huduma kwenye maeneo yao.

Aidha, Jaji Mkuu Masaju amesema Serikali inaendelea kuwasaidia wananchi wanaoshindwa kumudu gharama za uendesheji wa kesi kwa kutoa huduma ya  msaada wa kisheria  kupitia programu mbalimbali ikiwemo ya  "Samia legal Aid Project" ambapo wananchi ambao hawana uwezo wa kumudu gharama  wameweza kusaidiwa  huduma za kisheria

Ameongeza kuwa kasi ya usikilizwaji wa kesi imeongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi hiki cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan.

"Hivi karibuni kwenye hotuba yangu ya tarehe 22 Desemba  2025 nilisema tunaachana na utaratibu wakusubiria mashauri yaliyofunguliwa zamani yamalizike kwanza  ndipo tusikilize mapya, kesi itasikikizwa kwa kadri ya umuhimu na uwezo wake wakutatulika mapema, tulikuwa na utaratibu wa Mahakama ya mwanzo kukamilisha kesi kwa muda wa miezi sita,wilaya mwaka mmoja,Mahakama kuu na rufani kwa miaka miwili,kwa wakati huo tulikuwa na sababu za msingi, ikiwemo uchache wa Mahakimu na Majaji  na Mahakama chache,  lakini kwa sasa kesi zinatatuliwa kwa wakati sababu Mahakama zipo kila sehemu ya nchi" Amesisitiza Jaji Masaju.

Sambamba na hilo Jaji Masaju ameweka wazi kuwa Mahakama itaendelea kutoa Haki kwa usawa , uwazi   na uwajibikaji ili kuendana na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi