Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa wingi wa gesi – Waziri Kalemani
Sep 30, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_36030" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mkoani Mtwara, Septemba 27, 2018. Pamoja naye ni viongozi mbalimbali wa Serikali, TPDC na Kampuni ya Dangote.[/caption]

Na Veronica Simba – Mtwara

Imeelezwa kuwa Tanzania ina kiwango kizuri cha gesi asilia kinachofikia futi za ujazo trilioni 57.54, ambacho kinaipa nafasi ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki kwa wingi wa gesi kwa sasa.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, Septemba 27 mwaka huu, mkoani Mtwara wakati akizindua awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote.

Waziri Kalemani alisema kwamba, kati ya futi hizo za ujazo trilioni 57.54; Serikali imepanga kutumia futi za ujazo trilioni 8.8 kwa ajili ya matumizi ya viwandani, kikiwemo Kiwanda cha Dangote.

[caption id="attachment_36031" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mkoani Mtwara, Septemba 27, 2018. Kulia ni Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Jani mstaafu Josephat Mackanja na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda.[/caption]

Alisema kuwa, kazi ya Serikali ni kuhamasisha matumizi sahihi ya rasilimali hiyo adhimu ili iwe na tija kwa uchumi wa nchi.

“Mpaka sasa ziko kampuni 39 nchi nzima zinazotumia gesi; Dangote inakuwa ya 40. Tunaendelea kuhamasisha kampuni zaidi zitumie gesi katika kuendesha shughuli zao za uzalishaji ili pamoja na mambo mengine, wapunguze gharama za uzalishaji, waongeze tija na hivyo kuendelea kulipa kodi zote stahiki za Serikali,” alifafanua Waziri.

Akifafanua zaidi, Dkt Kalemani alisema kuwa, kwa kupunguza gharama za uzalishaji, wawekezaji wanakuwa na uwezo wa kuongeza ajira kwa watanzania hivyo kukuza kipato chao na hata uchumi wa nchi kutokana na kulipa kodi stahiki kama inavyotakiwa.

[caption id="attachment_36032" align="aligncenter" width="900"] Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni inayojishughulisha na uendeshaji na usimamizi wa miundombinu ya gesi hapa nchini; ambayo ni Kampuni-tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Baltazari Mrosso, akiwasilisha taarifa kwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (Meza Kuu – katikati), wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mkoani Mtwara, Septemba 27, 2018.[/caption]

Akizungumzia zaidi kuhusu tija ambayo Serikali itapata kupitia mpango huo wa matumizi ya gesi katika Kiwanda cha Dangote, Waziri Kalemani alisema kuwa, punguzo la asilimia 40 la gharama za uzalishaji ambalo wawekezaji hao watapata, litawawezesha kulipa kodi stahiki kwa Serikali, kuwepo na uwezekano wa kupunguza bei ya saruji, kuongeza ajira na faida nyingine mbalimbali.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Kampuni hiyo kwa Waziri; Mtendaji wake Mkuu hapa nchini, Jagat Ralthee alisema kuwa, kabla ya matumizi ya umeme wa gesi, Kampuni ilikuwa ikitumia lita zinazofikia 160,000 za mafuta ya dizeli kwa siku, ambazo zinagharimu takribani shilingi milioni 315,000. Kwa matumizi ya gesi, watapunguza asilimia 40 ya gharama hizo.

Naye Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni inayojishughulisha na uendeshaji na usimamizi wa miundombinu ya gesi hapa nchini; ambayo ni Kampuni-tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Baltazari Mrosso, alimweleza Waziri Kalemani kuwa, Mradi husika utazalisha megawati 45 za umeme kutokana na gesi, ambao utatumika katika shughuli za uzalishaji wa Kiwanda cha Dangote pekee.

[caption id="attachment_36033" align="aligncenter" width="900"] Msimamizi wa Usambazaji wa Gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwanaidi Rashid (kushoto), akimweleza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye shati la bluu) na Ujumbe wake, namna gesi inavyopokelewa na kutolewa katika Toleo Namba 1 la gesi katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Mtwara, muda mfupi kabla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda hicho, Septemba 27, 2018.[/caption]

Akizungumza na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Waziri Kalemani aliwaeleza miradi mingine mikubwa ambayo Serikali inapanga kutekeleza katika Mkoa huo, ambayo ni pamoja na Mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa megawati 300 unaotarajiwa kuanza Mei, 2019.

“Tutausafirisha umeme huo kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, umbali wa kilomita 502 ili kuuingiza kwenye Gridi ya Taifa.”

Vilevile, alitaja Mradi mwingine utakaoanza kutekelezwa mwakani, kuwa ni wa kuzalisha umeme wa gesi wenye megawati 330 na kuusafirisha kutoka Somanga Fungu  hadi Kinyerezi, umbali wa kilomita 98.2 na kuuingiza kwenye Gridi ya Taifa pia.

[caption id="attachment_36034" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akikagua mtambo wa kupunguza mgandamizo wa gesi katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Mtwara, muda mfupi kabla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda hicho, Septemba 27, 2018.[/caption]

Aidha, Waziri alisema Serikali inapanga pia kuanzisha Mradi mwingine wa Kinyerezi III mwezi Julai, 2019 wa kuzalisha umeme wa megawati 600 utakaotekelezwa kwa awamu mbili. Alisema awamu ya kwanza (Kinyerezi III (1) itazalisha umeme wa megawati 300, na ile ya pili (Kinyerezi III (2) itazalisha megawati nyingine 300.

“Kwahiyo, ni matumaini yetu kuwa, ndani ya miaka miwili hadi mitatu ijayo, tutaongeza kwenye Gridi ya Taifa, takribani megawati 1,012 za umeme kutokana na rasilimali ya gesi,” alisema.

Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilianza kazi hapa nchini Agosti, 2015 ambapo kina uwezo wa kuzalisha Tani 2500 za Saruji kwa siku, sawa na Tani 75,000 kwa mwezi.

[caption id="attachment_36035" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akijadiliana jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote hapa nchini, Jagat Ralthee (kulia), wakati akikagua mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme muda mfupi kabla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda hicho, Septemba 27, 2018.[/caption] [caption id="attachment_36036" align="aligncenter" width="900"] Sehemu ya umati wa wananchi wa Kijiji cha Hiari mkoani Mtwara, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Septemba 27, 2018.[/caption] [caption id="attachment_36037" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto-walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kiwanda cha Saruji cha Dangote, baada ya kuzindua rasmi awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda hicho, Septemba 27, 2018.[/caption] [caption id="attachment_36038" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto-walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Hiari, Mtwara baada ya kuzindua rasmi awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Septemba 27, 2018. Kijiji cha Hiari ndipo kilipo Kiwanda hicho.[/caption] [caption id="attachment_36029" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto-walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wa mkoani Mtwara, baada ya kuzindua rasmi awamu ya kwanza ya matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote.[/caption]

(Picha zote na Veronica Simba)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi