Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania, Afrika Kusini Kuimarisha Biashara
Aug 15, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Immaculate Makilika- MAELEZO

Serikali za Afrika Kusini na Tanzania zimekubaliana kuimarisha uhusiano wa kibiashara kwa kuongeza fursa katika nchi zao ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

Akizungumza  leo Ikulu jijini Dar es Salaam, mara ya baada ya kufanya mazungumzo ya faragha na Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli,  Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema kuwa Tanzania na Afrika Kusini zimedhamiria kukuza uchumi wake kwa kuimarisha biashara pamoja na uwekezaji katika madini, afya, utalii, pamoja na ulinzi na usalama.

Rais Ramaphosa  alisema, “Tunapenda kuishukuru Tanzania kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa za mazao, ambapo imesaidia Afrika Kusini kuongeza kununua idadi ya mazao kutoka  kutoka Tanzania”.

Aliongeza kuwa, Tanzania na nchi yake zina fursa nzuri  na nyingi za uwekezaji, na hivyo amewakaribisha Watanzania kuwekeza Afrika Kusini.

Vile vile, Rais Ramaphosa alisema kuwa nchi zao zimeendelea kulinda amani na umoja wao, ili kuendelea kuimarisha mtangamano wa kisiasa na uchumi katika nchi za Afrika. Rais Ramaphosa  ameahidi  ushirikiano  na Rais Magufuli anayetarajiwa kuwa   Mwenyekiti wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), katika mkutano wake wa 39 utakaofanyika Agosti 18 na 19 mwaka huu.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema kuwa ziara ya Rais Ramaphosa nchini ni fursa nyingine ya kukuza na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

Rais Magufuli aliongeza  kuwa Tanzania na Afrika Kusini zinaongoza kwa kufanya biashara katika nchi za SADC ambapo mwaka 2018 kiwango cha biashara kilikuwa dola za Kimarekani bilioni 1.18 kutoka bilioni 1.1 mwaka 2017.

Rais Magufuli aliongeza, “Kiwango cha bishara kutoka Tanzania kwenda Afrika Kusini kimefikia milioni 743.72 ikiwa ni sawa na asilimia 70 ya mazao katika nchi za SADC, huku  kwa mwaka 2018 biashara kutoka Afrika Kusini kuja Tanzania ilikuwa dola za Kimarekani milioni 437.2 na mwaka 2018  Kituo cha Uwekezaji Tanzaia (TIC) kimesajili biashara 228 kutoka Afrika Kusini.”

Aidha, aliongeza kuwa nchi hizo zimejadili hatua mbalimbali za kuboresha biashara ikiwemo kukuza sekta ya viwanda, kupunguza utitili wa kodi na kuanzisha wizara mahususi ya uwekezaji.

Kuhusu kukuza sekta ya utalii, wamekubaliana kutangaza kwa pamoja vivutio vya utalii huku wakitarajia kuongeza utalii ambapo Afrika Kusini inaingiza watalii milioni 10 kwa mwaka na Tanzania watalii milioni moja pekee.

Katika sekta ya madini, Rais Magufuli alisema wamekubaliana kubadilishana uzoefu wa utaalamu wa madini, kujenga viwanda vya kuchakata pamoja na kuongeza thamani ya madini.

Aidha, Afrika Kusini imekubali kutoa mafunzo ya kitaalamu katika masuala ya ulinzi kutoka nchini Tanzania.

Rais Cyril Ramaphosa amewasili nchini jana usiku kwa ziara ya kikazi ambapo kesho Agosti 16, anatarajiwa kutembelea kambi za wapigania uhuru zilizopo Mazimbu mkoani Morogoro, na baadae anatarajiwa kuhudhuria Mkutano wa 39 wa Wakuu wa nchi za SADC.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi