Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tani 2 za Bidhaa Zenye Thamani ya Milioni 20 Zateketezwa na TBS
Aug 20, 2020
Na Msemaji Mkuu

Afisa Mdhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati, Sileja Rushibika (kushoto) na Afisa Usalama wa Chakula wa shirika hilo Kanda ya Kati, Vicent Meleo (kulia) wakikagua baadhi ya bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na zilizokatazwa kutumika kabla ya kuteketezwa katika dampo la chidaya mjini Dodoma.

Na Jacquiline Mrisho

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza jumla ya tani 2.2 za bidhaa zilizoisha muda wake na zilizokatazwa kutumika zenye thamani ya shilingi 20,150,000.

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dodoma na Afisa Mdhibiti Ubora wa shirika hilo Kanda ya Kati, Sileja Rushibika wakati alipokuwa akisimamia zoezi la uteketezaji wa bidhaa hizo.

Rushibika amesema kuwa zoezi la kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingia sokoni vikiwemo vyakula na vipodozi ni jukumu la kawaida na lipo kwa mujibu wa Sheria ya Viwango na Sheria ya Fedha.

                                                                                                                                              “Leo tumeteketeza jumla ya tani 2.2 ambapo kati ya bidhaa hizo, kilo 1200 ni vyakula vilivyomaliza muda wake ambavyo thamani yake ni shilingi milioni 6, kilo 820 ni vipodozi vilivyoisha muda wake vyenye thamani ya shilingi milioni 10 pamoja na kilo 180 za vipodozi vilivyokatazwa vyenye thamani ya shilingi 4,150,000”, alisema Rushibika.

Afisa Mdhibiti Ubora wa shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati, Sileja Rushibika akisaidia kukusanya bidhaa ambazo zimeisha muda wa matumizi na zilizokatazwa kutumika zikiwa tayari kwa kuteketezwa katika dampo la chidaya lililopo jijini Dodoma.
 

Rushibika ametoa rai kwa wafanyabiashara ambao sio waaminifu wanaouza bidhaa zilizokataliwa au kuisha muda wake kuacha tabia hiyo na badala yake wazitenge na kufuata utaratibu wa shirika hilo wa kuziteketeza.

Aidha, wananchi wanatakiwa kuwa na jadi ya kusoma muda wa matumizi ya bidhaa kabla hawajanunua kwa sababu bidhaa zote zimeandikwa.

Buludoza likiendelea na kazi ya kuteketeza bidhaa zilizoisha muda wake na zilizokatazwa kutumika zilizokamatwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Amesisitiza kuwa, suala la kudhibiti ubora sio la TBS pekee bali wananchi wanaweza wakashiriki hata kwa kutoa taarifa ili shirika liweze kufuatilia hali itakayopunguza gharama zisizo za lazima kwa Serikali.  

Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula wa TBS Kanda ya Kati, Vicent Meleo, amewasisitiza wananchi kuacha matumizi ya vipodozi vilivyokataliwa kwa sababu vinaharibu ngozi zao na kusababisha saratani, amewataka pia kutotumia dawa kama vipodozi na badala yake wafuate ushauri wa wataalam wa afya.

Zoezi la ukaguzi wa bidhaa hizo ni endelevu, zoezi hilo limefanyika katika Mikoa ya Singida, Tabora na Dodoma.  

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi