Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TANESCO Imetekeleza Mikakati ya Kumaliza Tatizo la Umeme Dar es Salaam, Pwani.
Feb 12, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na. Msafiri Ulimali

Utekelezaji wa miradi ambayo itaisaidia Tanzania kufikia “Tanzania ya Viwanda” unazidi kutoa nuru, ambapo Serikali imejikita zaidi katika kutengeneza miundombinu rafiki ya kuzalisha umeme wa uhakika, Juhudi hizi za Serikali zilijikita zaidi vijijini; mradi wa umeme vijijini, sasa kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kadhia ya umeme kwa wakazi na viwanda vya jiji la Dar es salaam na Mkoa wa Pwani inakwisha.
Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kuweza kusimika Transfoma yenye uwezo wa MVA 300 sawa na Megawati 240, Ubungo, jijini Dar es Salaam, imepamba moto chini ya  Mkandarasi  wa ABB kutoka Switzerland, huku TANESCO ikisema ufungwaji wa Tranforma utaanza februari, 22 na wanatarajiwa kukamilisha rasmi  mwezi Mei mwaka huu.
Chombo hicho kitaongeza nguvu katika kituo cha umeme cha Ubungo kutoka MVA 300 hadi 600, sawa na MW 480, hapana shaka ni taarifa njema katika miji hii miwili kwani sasa wataondoka katika umeme wa mashaka na kuwa katika mwanga tosha na mahitaji ya viwandani kwa maendeleo ya jamii; majumbani na maofisini, pia ukuzaji wa uchumi wa viwanda na biashara.
Afisa Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji anaeleza, “kuongezeka mahitaji ya umeme katika Mkoa wa Dar e salaam na Pwan, Serikali ya Awamu ya Tano, imeona kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza nguvu ya umeme katika Mkoa wa Dar es salaam Pwani.”
Idadi ya watu, hususani kwa Mkoa wa Dar es Salaam inachangia kama sababu kubwa ya hitaji hilo la nishati ya umeme, inaelezwa kuwa Mkoa wa Dar es salaam pekee una jumla ya wakazi wapatao 5,465,420 huku Mkoa wa Pwani ukiwa na jumla ya 1,098,668; hawa wote wanahitaji nishati hiyo.
Msemaji huyo wa Tanesco alieleza kuwa hapo awali kituo cha umeme cha Ubungo kilikuwa na transfoma mbili ambazo kila moja ilikuwa na uwezo wa kutoa umeme wa MVA 150, na kuwa ongezeko la transfoma mpya itafikisha MVA 600, “kihesabu unaweza kusema ni ndogo, kifizikia ni nguvu kubwa itakayotoka hapo.” Alisema Leila
Ongezeko la idadi ya viwanda katika Mkoa wa Pwani ni moja ya sababu ya ujio wa Transfoma hiyo, kwa sasa Pwani inaonekana kama ndio Mkoa wenye viwanda vingi na vikubwa ukianzia Mkuranga, Kisarawe, Kibaha Mjini, Rufiji ,Mafia, Kibiti, Bagamoyo mpaka Chalinze, maendeleo haya  makubwa ya uanzishwaji wa viwanda unachochea ongezeko la uhitaji wa nishati ya umeme.
Katika kipindi cha mwaka 2018 Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeweza kupata, mafanikio makubwa katika uboreshaji wa miondombinu ya usamabazaji wa umeme katika pande zote nchini kutokana na miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikiendelea.
Kazi hiyo kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inaonyesha dhahiri dhamira ya kuondoa tatizo la umeme nchini ili kuondoa kadhia ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi.
Akifafanua kuhusu uwezo wa Transfoma hiyo, Mkuu wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme Ubungo, Mhandisi Joseph Msumali amesema uwezo wa kusukuma takribani Megawati 240 kutoka kwenye msongo wa Kilovoti 220 kuelekea Msongo wa Kilovoti 132 kwa ajili ya usambazaji na matumizi ya nishati ya umeme katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Hata hivyo ilikuwa ni kawaida kuona matangazo kwenye vyombo vya habari TANESCO ikiomba radhi kukatika kwa umeme mara kwa mara katika maeneo ya Pwani na Dar es Salaam, kwa kuhakikisha huduma zinapatikana, Shirika la Umeme Tanesco limeweza kuanza na mradi mpya ujulikanao Mradi wa kuimarisha Mifumo ya usambazaji umeme (TEDAP).
“huenda ikawa ni mara ya kwanza kusikia, hawa TEDAP wanajishughulisha na uondoaji wa mifumo yote ya zamani na kufanya ukarabati,” Afisa Mahusiano, TANESCO alifafanua.
Mifumo mingi ya usambazaji ya umeme imekuwa chakavu jambo ambalo TEDAP imekuja na utaratibu wa kuhakikisha wanarekebisha kabla ya kutokea tatizo kubwa, na kwa sasa wameweza kufanikisha ukarabati sehemu mbalimbali ndani ya Mkoa wa Dar es salaam kwa asilimia 98, katika maeneo kama Mbagala, Gongo la Mboto, Kurasini pamoja na Kipawa, na mradi TEPAD uko kwenye hatua za mwisho.
Pamoja na jitihada za kukarabati, Tanzania imebarikiwa kuwa na nishati ya gesi ambapo miradi mingi mikubwa inatekelezwa kwa kasi ili nchi ifanikiwe kuwa na umeme wa kutosheleza hasa kwenye miradi mipya ya viwanda na reli ya kisasa (SGR),Pia na mahitaji ya jamii kwa ujumla.
Kwa sasa miradi mingi imekamilika kwa asilimia kubwa kama vile Mradi wa Kinyerezi 1 na Kinyerezi 2, huku kinyerezi 1 wenye jumla ya MW 150 ukipanuliwa ili kuongeza MW 180, zingine ambapo jumla ya MW 340 zitazalishwa, ikumbukwe kuwa nishati ya umeme wa gesi ni teknolojia mpya nchini  itakayoweza kuzalisha  umeme na kupunguza gharama za umeme nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanesco Dkt. Tito Mwinuka katika mkutano wake na wahariri Mkoani Arusha alionesha maono yake ya kuliona Shirika hilo likijiendesha kifaida zaidi, huku akionesha baadhi ya kazi ambazo zimeshaanza kufanyika na nyingine kukamilika.
“Huwa nasema mbele ya wafanyakazi wenzangu, kwamba ningependa kuona TANESCO ambayo inafanya kazi kwa ufanisi na ndiko tunakokwenda, ndoto yangu ni kuona TANESCO inajiendesha kwa faida", Dkt. Mwinuka.
Mbali na maono hayo, Dkt. Mwinuka amehakikisha upatikanaji wa umeme katika maeneo muhimu ili kuhakikisha uendeshaji usiodorora katika viwanda ili bidhaa za viwanda vyetu ziweze kushindana katika soko la kimataifa.
 “Katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme kama nguzo muhimu ya ujenzi wa Tanzania yenye viwanda, Serikali kupitia TANESCO hivi sasa inatekeelza miradi mikubwa ya umeme 22 kwa wakati mmoja na kwa fedha za Serikali.”Dkt. Mwinuka- Mkurugenzi Mtendaji TANESCO.
Tanesco imeendelea na utekelezaji wa miradi ya umeme ukiwemo ujenzi wa mradi wa Kinyerezi 1 extension MW 185, ufungaji wa mitambo na kukamilisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme ambapo shilingi bilioni164 fedha za ndani zimetengwa.
Huku miradi mengine ianyoendelea kutekelezwa ni Mradi wa kuzalisha umeme Rusumo wa MW 80, Mtwara Power Project MW 300, Somanga Fungu MW 330 pamoja na Mradi wa Kakono MW 87.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi