Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAKUKURU Arumeru Yaagizwa Kusaidia Elimu ya Rushwa kwa Wanafunzi
Sep 03, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Prisca  LIbaga-Arumeru.

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru), Wilayani Arumeru imeagizwa kuwaandalia makongamano ya kutoa elimu ya mapambano ya rushwa  Klabu ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Mwandeti, iliyopo wilayani Arumeru Mkoani Arusha.

Agizo hilo limetolewa Septemba 3 na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour, aliyetembelea shule hiyo alipokuwa akizindua bweni jipya la wasichana lililojengwa kwa nguvu za wananchi na serikali

Amesema amevutiwa na Klabu hiyo ya wanafunzi ambayo imekuwa ikielimisha walimu, wanafunzi wa shule hiyo na wananchi kuhusu madhara ya rushwa hivyo Takukuru iwawezesha na apewe taarifa.

Amour, amesema rushwa ni adui wa haki na penye rushwa hakuna haki wala amani wala maendeleo na rushwa ni chanzo cha kukosekana kwa maadili hivyo akaitaka Takukuru kuilea Klabu hiyo kwani wanafunzi hao wanafanya kazi kubwa ya kuelimisha madhara ya rushwa.

Kuhusu elimu, amewataka wakuu wa shule zote nchini kuhakikisha wanasimamia taalumua ipasavyo ili wanafunzi waweze kupata elimu bora badala ya bora elimu na kuwataka walimu watambue kuwa wakati wa kufanya kazi kwa mazoea umepitwa na wakati hivyo lazima wabadilike.

Amempongeza Mkuu wa Shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha sita, Mwalimu John Massawe kwa kusimamia nidhamu na taaluma na hivyo wanafunzi wanapata elimu sahihi inayostahili.

Katika hatua nyingine Amour amemuagiza mkandarasi anayejenga tanki la maji katika kitongoji cha Ekenywa, kata ya Olturumet, kufanya ukarabati wa ufa uliopo kwenye tanki hilo ili liweze kuhifadhi maji na kuwanufaisha zaidi ya wananchi 3750.

Aidha amewaonya makandarasi wote nchini kuacha kutekeleza miradi hiyo chini ya viwango na kuzitaka halmashauri kuhakikisha zinasimamia kwa karibu miradi yote ili iwanufaishe wananchi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander  Mnyeti, amesema mwenge wa Uhuru ukiwa wilaya ya Arumeru yenye Halmashauri mbili za Arusha DC na Meru, utazindua miradi sita yenye thamani ya shilingi bilioni 3.735.

Akipokea mwenge wa Uhuru  katika kijiji cha Oldonyosambu, kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo, Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mnyeti, ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na Elimu, Afya, Kilimo, Ufugaji samaki, Viwanda, Mazingira Uvuvi, Mifugo na maji .

Mnyeti ametumia fursa hiyo kumpongeza mwekezaji  wa kiwanda cha kutengeneza vifungashio vya bidhaa vinavyozalishwa kutokana na malighafi kutoka kiwanda cha Karatasi cha Mgololo, Mkoani Iringa, Prospa Swatty na kusema vifungashio hivyo vinaongeza samani za bidhaa .

Amesema kiwanda hicho ambacho kinamilikiwa na Mzawa ni mkombozi  kwa wafanyabiashara ambao walikuwa wakizalisha bidhaa zao na kugiza vifungashio kutoka nje na  kupitia kiwanda hicho wafanyabiashara nchini hawatalazimika tena kuagiza vifungashio hivyo kutoka nje .

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi