Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TADB Kuanzisha Bima ya Kilimo na Afya kwa Wakulima.
Sep 11, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_13117" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Mikopo na Usimamizi wa Biashara kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Augustine Chacha akifafanua jambo wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari kuhusu mikopo inayotolewa na benki hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw.Francis Assenga. (Picha na: Idara ya Habari - MAELEZO)[/caption]

Na: Agness Moshi 

Benki  ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imejipanga kuanzisha mfuko wa bima kwa ajili ya wanufaika wa mikopo wa banki hiyo ili kuwawezesha kumudu gharama za afya na kukabiliana na  changamoto za kilimo zinazoletwa na mabadiliko ya tabia nchi kama vile ukame na mafuriko.

Akiongea na wandishi wa habari  jijini  Dar Es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw.Francis Assenga amesema benki hiyo iko kwenye mchakato wa kuanzisha mfuko wa bima kwa wakulima utakaounganishwa  moja kwa moja na Mfuko wa Taifa  wa Bima ya Afya (NHIF)  ili kuwawezesha wakulima kuwa na afya bora na kuwahakikishia usalama wa mazao yao kuanzia yanapokuwa shambani hadi yanapofika sokoni.

Aliongeza kusema kuwa bima zitakazotolewa kupitia benki hiyo zitakuwa za aina tatu ambazo ni bima ya maisha ambayo ni kwa ajili ya mkulima na benki endapo kutatokea vifo, bima ya afya kwa ajili ya mkulima na familia yake itakayowawezesha kumudu gharama za matibabu na bima ya mazao ambayo itahusisha mazao kuanzia shambani, usafirishaji, uhifadhi na sokoni.

“Kwa kweli ni matamanio yetu kuona mkulima anaendelea sio tu kwa kupata fedha nyingi au mazao mengi bali anaendelea katika maisha yake kiujumla ikiwa ni pamoja na kuhakikisha yeye na familia yake wana afya njema”, alisisitiza  Bw.Assenga.

Aidha, ameongeza kuwa, bima hizi zitamhakikishia mkulima usalama wa mazao yakiwa shambani na ghalani, usalama wa afya yake pamoja na familia yake  na zitamsaidia kulipa mkopo endapo kutatokea mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanaweza kumkwamisha kulipa mkopo  na endapo  kifo kitatokea bima itashughulika katika ulipaji wa mkopo.

Alisisitiza kuwa, benki hiyo inafanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo tayari wameshaanzisha mchakato wa kutengeneza mazao ambayo yatahusisha kilimo na bima za afya ambao utawahakikishia  wakulima kupatiwa huduma za afya.

 Bw.Assenga ametoa wito kwa wadau wenye nia ya kuanzisha miradi mikubwa itakayohusisha sekta ya kilimo na  mabadiliko ya tabia  nchi kuwasiliana na benki hiyo ili waweze kupatiwa mikopo ambayo itawawezesha kutekelezea miradi hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Mikopo na Usimamizi wa Biashara kutoka Benki hiyo Augustine Chacha amesema kuwa benki hiyo inafanya kazi na taasisi yoyote au mtu yoyote atakayeweza kusaidia wakulima wadogo kujiendeleza ili kujikwamua kutoka katika kilimo cha kijikimu na kwenda katika kilimo cha biashara.

“Tunataka wawekezaji waje tuwape pesa watengeneze miradi itakayowawezesha kuwasaidia wakulima wadogo ili kuleta mapinduzi ya kilimo na kukifanya kuwa kilimo cha biashara “ alisema Chacha.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilianza rasmi mwaka, 2015 ikiwa na lengo la kusaidia upayikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu ikiwa ni pamoja na kuchagiz na kusaidia mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kijikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi