Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taasisi Zinazohusika na TEHAMA Zatakiwa Kushirikiana Kuendeleza Vipaji
Mar 13, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_41231" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wadau pamoja na wanafunzi wa kike (hawapo pichani) jana jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo na mashindano ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA yaliyoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.[/caption]

Na Jacquiline Mrisho.

Taasisi zinazohusika na Masuala ya TEHAMA nchini zimetakiwa kuendelea kushirikiana katika kuinua vipaji vya wanafunzi wanaosoma masomo yahusuyo TEHAMA na kuviendeleza ili viweze kuondoa changamoto zilizopo katika jamii.

Hayo yamesemwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akifunga mafunzo na mashindano ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA yaliyoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.

Prof. Ndalichako amesema kuwa nia ya Serikali ni kuona mchango wa Sayansi na Teknolojia ukiongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za jamii na kuongeza tija katika uzalishaji hususani katika sekta zinazogusa wananchi moja kwa moja zikiwemo za uchumi, kilimo, mifugo na viwanda.

“Hadi sasa tunaona mafanikio mengi ya matumizi ya TEHAMA ambapo hata wajasiriamali wamekuwa wakikuza biashara zao kupitia mitandao, pia mapato ya serikali yameendelea kuongezeka baada ya kuingia kwenye mfumo wa matumizi ya TEHAMA hivyo kutokana na mafanikio hayo, natoa rai kwa wadau wote wa TEHAMA kushirikiana na Serikali sio tu kuinua vipaji bali na kuviendeleza,” alisema Prof. Ndalichako.

[caption id="attachment_41232" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akimvalisha medali mwanafunzi Monica Cleophance ambaye ni kati ya wanafunzi 6 waliopata nafasi ya kwenda nchini Ethiopia kwa ajili ya kushiriki fainali za mashindano hayo ya watoto wa kike ulimwenguni.[/caption]

Prof. Ndalichako amefafanua kuwa Serikali imeendelea kutoa msisitizo katika masuala ya TEHAMA ambapo hivi karibuni imetoa  jumla ya Kompyuta 300 na Projekta 100 kwa ajili ya kuendeleza mafunzo ya teknolojia, habari na mawasiliano kwenye Vyuo vya Walimu pia zimeanzishiwa maabara za kompyuta kwa baadhi ya shule ili kuendeleza mafunzo ya teknolojia hiyo.

Ametoa rai kwa wanafunzi kuacha kuitumia vibaya TEHAMA na badala yake kusoma masomo hayo kwa kuwa fursa za masomo ya Sayansi na Teknolojia ni nyingi pia zinatoa nafasi kwa watu kujiajiri kwa kutengeneza programu mbalimbali ambazo zinaweza kuuzwa kwa gharama kubwa.

Akiongelea kuhusu mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, (UCSAF) Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA ilianzishwa kwa lengo la kumuhamasisha mtoto wa kike kuchagua masomo ya TEHAMA na kuweza kupata fursa katika sekta hiyo.

[caption id="attachment_41233" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akifurahi pamoja na mwanafunzi Khatija Saphy baada ya mwanafunzi huyo kuwa mmoja kati ya washindi sita na kupokea zawadi ya kikombe, kompyuta mpakato na kupata safari ya kwenda nchini Ethiopia kwa ajili ya kushiriki fainali za mashindano hayo ya watoto wa kike ulimwenguni.[/caption]

“Kama Taifa tunajiandaa kuelekea katika uchumi wa kati ambao ni uchumi wa viwanda hivyo hatuna namna yoyote ya kuufikia uchumi huo kama hatutowaelimisha wananchi kuhusu masuala ya TEHAMA, Sayansi na Teknolojia, tunaamini kuwa ukimuwezesha mtoto wa kike basi umeelimisha familia na Taifa ndio maana tunawahamasisha kusoma masomo hayo,” alisema Mhandisi Ulanga.

Akiwakilisha wanafunzi wenzie, Khatija Saphy ameishukuru Serikali kwa kutoa motisha hiyo ya wanafunzi wa kike kupenda masomo ya sayansi, ameiomba Serikali kuendelea kutoa fursa hizo mpaka vijijini kwa sababu maeneo hayo yana wanafunzi wengi wabunifu ambao hawapati nafasi hiyo.

Juhudi za Mfuko huo juu ya kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya Sayansi zilianza tangu mwaka 2016 ambapo kila mwaka wanafunzi 248 wa kidato cha tatu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani hasa wanaopata daraja la kwanza kwenye mitihani ya  kidato cha pili wanapata fursa ya kupata mafunzo ya TEHAMA hasa namna ya kutengeneza mifumo ya komputa.

Vile vile ili kuongeza hamasa, wanafunzi 31 wanapewa medali na wanafunzi sita kati ya hao wanapata zawadi za kikombe, kompyuta mpakato na safari ya kwenda nchini Ethiopia kwa ajili ya kushiriki fainali za mashindano hayo ya watoto wa kike ulimwenguni.

[caption id="attachment_41234" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na wanafunzi wa kike 31 waliopata mafunzo hayo. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Mhandisi Peter Ulanga[/caption]      

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi