Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taasisi za Serikali Zatakiwa Kulipa Madeni TANESCO
Sep 18, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_47029" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa nne kushoto) akiwasha umeme katika Kijiji cha Gasuma wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.[/caption]

Na Hafsa Omar

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ameziagiza taasisi za Serikali zenye madeni ya umeme zihakikishe kuwa zinalipa madeni hayo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ili Shirika hilo liendelee kutoa huduma bora kwa watanzania wote.

Alitoa agizo hilo Septemba 17 mwaka huu, wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Gasuma, wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu wakati alipoenda kuwasha umeme kwenye kijiji hicho.

Aidha, Naibu Waziri alisema kuwa, Shirika hilo limepewa jukumu la kusaidiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kusambaza umeme katika maeneo yote ambayo bado hayajafikiwa na umeme nchini ifikapo Juni 2021 hivyo ikiwa wateja wake hawatalipa madeni yao ndani ya muda stahiki, Shirika hilo halitafanya kazi kwa ufanisi.

[caption id="attachment_47030" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Gasuma wilayani Bariadi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu wakati alipofika kijijini hapo kuwasha umeme.[/caption]

“Meneja wa Mkoa,  endelea kuchukua hatua za kisheria, nimeona tayari umeshaanza kuchukua hatua hizo, lakini hazitoshi deni linazidi kukua endelea kuwachukulia hatua wale wote ambao hawajalipa madeni yao.’’Alisema Mgalu

Pia aliwaagiza, Wakuu wa Wilaya kulichukua  suala hilo la madeni ya umeme kwenye taasisi za Serikali kama moja ya  ajenda zao katika vikao vyao vya kila siku, kwani madeni yao yanaweza kusababisha Shirika hilo likashindwa kujiendesha lenyewe.

Alifafanua kuwa, kwa sasa Shirika hilo linajitegemea lenyewe na halipokei ruzuku tena kutoka Serikalini na Wizara ya Nishati haitaki kuona Shirika hilo linafikia hatua ya  kuomba tena  ruzuku ili kujiendesha.

[caption id="attachment_47031" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya wananchi, wilayani Itilima, Mkoa wa Simiyu wakimlaki Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alipofika wilayani humo kuwasha umeme katika Kijiji cha Mwamanyangu na Mwanunui.[/caption]

Kuhusu mahitaji ya umeme katika Mkoa wa Simiyu, alisema kuwa, mkoa huo unahitaji umeme wa kutosha ili kutimiza lengo la Mkoa la ujenzi wa viwanda hivyo katika mwaka huu wa fedha, Serikali imeamua kujenga kituo cha kupoza umeme, kazi ambayo imekwishaanza.

‘Mkoa huu ni mkoa unaojenga  viwanda, kwahiyo mahitaji yanaongezeka, umeme uliopo hautatosha lazima tujenge kituo cha ambacho kwakweli kitaweza kupokea umeme na kupooza na kusambaza katika maeneo mengine na kazi hiyo imeanza.’’Alisema Mgalu

Katika ziara yake mkoani Simiyu, Naibu Waziri pia aliwasha umeme katika vijiji vya Mwamanyangu na Mwanunui katika wilaya ya Itilima.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi