[caption id="attachment_38484" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akielezea mikakati ya Wizara ya Madini katika kuboresha shughuli za uchimbaji mdogo wa madini kwenye mkutano wa hadhara wa wachimbaji wadogo wa madini uliofanyika katika tarafa ya Mang’onyi iliyopo wilayani Ikungi mkoani Singida.[/caption]
Na Greyson Mwase, Singida
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameuagiza Mgodi wa Dhahabu wa Shanta uliopo katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida kuhakikisha unatoa taarifa za tafiti zake zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ili wachimbaji wadogo waweze kuzitumia katika kubaini madini yaliyopo na kuanza kuchimba kwa kufuata sheria na kanuni za madini.
Naibu Waziri Biteko alitoa agizo hilo leo tarehe 19 Novemba 2018 kwenye mkutano wa hadhara na wachimbaji wadogo wa madini uliofanyika katika tarafa ya Mang’onyi wilayani Ikungi mkoani Singida kama sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wachimbaji wa madini
[caption id="attachment_38483" align="aligncenter" width="750"] Kutoka kulia, Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu walisikiliza kero mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wachimbaji wadogo kutoka katika tarafa ya Mang’onyi iliyopo wilayani Ikungi mkoani Singida kwenye mkutano wa hadhara. (hawapo pichani).[/caption]Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mazingira bora ya uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kuwapatia taarifa mbalimbali za utafiti zilizofanywa na Wakala wa Utafiti na Jiolojia Tanzania (GST) na kampuni za utafiti wa madini lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa uchimbaji wao unakuwa wa uhakika na sio wa kubahatisha.
Akielezea maboresho mengine yaliyofanywa katika sekta ya madini, Biteko alisema Serikali imeboresha Sheria ya Madini inayotambua madini kama mali ya watanzania yanayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali imeweka mkakati wa kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini wasio rasmi na kuwapatia leseni za madini ili uchimbaji wao ulete tija kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
[caption id="attachment_38482" align="aligncenter" width="750"] Wananchi wa tarafa ya Mang’onyi iliyopo wilayani Ikungi mkoani Singida wakisikiliza ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.[/caption]Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi na kupewa leseni ili waanze kuchimba na kulipa kodi serikalini.
“Sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Madini lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunaweka mazingira bora kwa wachimbaji wadogo wa madini ili uchimbaji uongeze kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia kodi na tozo mbalimbali,” alisema Biteko.
Wakati huohuo Biteko aliwataka wananchi wanaoishi karibu na Mgodi wa Dhahabu wa Shanta kutokuharibu miundombinu ya maji iliyowekwa ili iweze kunufaisha wananchi wote.
Awali wakiwasilisha kero mbalimbali wakazi hao waliiomba Wizara ya Madini kuwapatia maeneo kwa ajili ya uchimbaji wa madini ili waweze kujiingizia kipato na kulipa kodi serikalini.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wadogo wa madini katika tarafa ya Mang’onyi iliyopo wilayani Ikungi mkoani Singida, Consolata Joseph alisema kuwa uchimbaji wao umekuwa ni wa kubahatisha na hata kuvamia maeneo yenye leseni kubwa ya madini inayomilikiwa na Kampuni ya Dhahabu ya Shanta.
Aliongeza kuwa, kama wachimbaji wadogo wapo tayari kulipa kodi stahiki serikalini mara baada ya kupatiwa maeneo na kuanza kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini.
Awali akizungumza katika ziara hiyo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Shanta uliopo wilayani Ikungi mkoani Singida, Philbert Rweyemamu alisema mgodi umeshaanza kutoa fidia na kuongeza kuwa mpaka sasa umeshatoa shilingi bilioni 2.6 pamoja na ujenzi wa makazi mbadala ambapo mpaka sasa wameshajenga nyumba sita.
Aliongeza kuwa mpaka ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu, mgodi unatarajia kukamilisha ujenzi wa nyumba nyingine sita na kufanya idadi ya nyumba kuwa 12 kama sehemu ya kuhakikisha wananchi wanaolipwa fidia wanaishi katika mazingira mazuri.
Akizungumzia changamoto za mgodi wake, Rweyemamu alieleza kuwa ni pamoja na wachimbaji wadogo haramu kuvamia eneo la mgodi na kuchimba madini, miundombinu kuhujumiwa na baadhi ya wananchi kugomea fidia inayotolewa na kampuni hiyo.