Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TEWW yatoa suluhisho kwa waliokosa fursa
May 31, 2021
Na Msemaji Mkuu

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ni Taasisi ambayo pamoja na majukumu mengine inaandaa wataalamu wa Elimu ya Watu Wazima nchini.  Ili kutimiza jukumu hili TEWW ina programu ya Elimu ya watu wazima na Maendeleo ya jamii, pia elimu ya watu wazima na mafunzo endelezi  katika ngazi ya Astashahada, stashahada na Shahada kwa njia ya ana kwa ana pamoja na kwa njia ya masafa.

 Mafunzo ya Shahada ya Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelezi pamoja na Shahada ya Elimu ya Watu Wazima  na Maendeleo ya Jamii yanatolewa katika kampasi ya Dar es Salaam huku stashahada ya Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelezi na Maendeleo wa Jamii kutolewa katika kampasi ya Dar es Salaam, Luchelele - Mwanza na WAMO - Morogoro na Mafunzo ya Elimu masafa kwa njia ya masafa inatolewa katika mikoa yote ya Tanzania Bara’ alisema Bw. Justine Mbwambo ambaye ni Mhadhiri Msaidizi na Afisa Udahili wa TEWW.

Hivyo basi, TEWW inaandaa wataalamu  wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi nchini ambao wana jukumu la kuanzisha, kutekeleza na kusimamia mipango na miradi mbalimbali ya kielimu katika jamii. Aliongeza Bw. Mbwambo

Nae, Bi. Leonia Kassamia ambae ni Mkuu wa kitengo cha Elimu kwa Umma na Maendeleo ya Wanawake toka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) amesema TEWW imekuwa  ikianzisha na kusimamia mipango na miradi ya kielimu inayolenga makundi tofauti tofauti ya jamii ikiwemo vijana, watu wazima, wanawake na makundi mengine yenye mahitaji  mbalimbali ya kielimu, ‘TEWW ndio mwarobaini kwa watanzania wote ambao hawakufanikiwa kupata fursa ya kujiendeleza katika mfumo rasmi wa Elimu Tanzania Bara’ Aliongeza.

TEWW imekuwa na miradi mbalimbali ambayo inaitekeleza ambayo ni Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana (MECHAVI), Elimu Changamani Baada ya Msingi (MECHAM), Elimu ya Sekondari nje ya mfumo rasmi pamoja na kuwawezesha wasichana na wanawake walio nje ya shule kupata elimu kulingana na mahitaji.

Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana (MECHAVI) walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ‘Integrated Program for out of School Adolescents’ maarufu kama IPOSA ni mradi unaolenga kutoa stadi za kisomo (kusoma, kuandika na kuhesabu), ujasiriamali, stadi za kazi na stadi za maisha. Hii ni kutokana na kubainika kuwa kuna vijana wa umri wa miaka 14-17 wapatao milioni 3.5 (sense 2012) ambao hawako shuleni na hapakuwepo na programu thabiti ya kuwahudumia.

Bi. Kassamia ameongeza kuwa, Mpango wa IPOSA unawalenga vijana wa kike na wa kiume ambao hawajawahi kwenda shule kabisa na wale walioacha shule za msingi au kumaliza darasa la saba bila ya kuwa na stadi muhimu na za msingi katika maisha. Mpango huu unatekelezwa kwa majaribio katika mikoa 8 ambayo ni Kigoma, Dar es Salaam, Songwe, Tabora, Dodoma, Njombe, Mbeya na Iringa.

Programu nyingine inayotolewa na TEWW ni Elimu Changamani Baada ya Msingi (MECHAM) au Integrated Post Primary Education (IPPE). Programu hii inawalenga vijana na watu wazima waliomaliza elimu ya msingi. Hii ni programu changamani inayounganisha maeneo matatu ya kujifunzaji ambayo ni ufundi wa awali, stadi nyenzo na taaluma ili kuwafanya walengwa waweze kumudu maisha yao na kujitegemea kwa kuanzisha shughuli za maendeleo.

TEWW pia inatoa na kusimamia utoaji wa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi na kuratibu wadau mbalimbali wanaotoa huduma hii nchini. Ni katika programu hii ambapo mradi wa kutoa elimu kwa wasichana walioacha shule kwa ajili ya ujauzito unatekelezwa.

Miradi mingine ni pamoja na kuwawezesha wasichana na wanawake walio nje ya shule kupata elimu kulingana na mahitaji yao ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuendeleza biashara. Mradi huu unatekelezwa katika wilaya za Sengerema, Ngorongoro na Kasulu. Pia tuna mradi wa kusindika minofu ya samaki katika kituo chetu cha Luchelele Mwanza.

Ikumbukwe kuwa, TEWW ni Taasisi ya Umma ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na ilianzishwa na Sheria ya Bunge namba 12 ya Mwaka 1975 pamoja na majukumu mengine ikiwa ni kuwaandaa wataalamu wa Elimu ya Watu Wazima, kuandaa mipango na programu mbalimbali ya kuendeleza elimu ya Watu Wazima ambapo inawezesha kuifanya Tanzania ya Viwanda.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi