VIPAUMBELE VYA SEKTA YA ELIMU KAMA ILIVYOAINISHWA KATIKA ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) 2015/20 NA MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO 2015/2020
Ilani ya CCM inaipa kipaumbele Sekta ya Elimu umuhimu wa kipekee ili kuiendeleza sekta hii. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2015-2020), CCM itahakikisha Serikali inasimamia Utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 kwa kutekeleza yafuatayo:-
- Kuandaa mfumo, muundo na taratibu nyumbufu za kutoa Elimu ya Awali na Elimumsingi (1+6+4) bila malipo ili kuhakikisha kwamba:-
- Uandikishwaji rika lengwa la watoto wa darasa la Elimu ya Awali unaongezeka kutoka asilimia 45 mwaka 2015 hadi asilimia 100 mwaka 2020
- (ii) Uandikishwaji rika lengwa la watoto wa Darasa la Kwanza unaongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2015 hadi asilimia 100 mwaka 2020; na
- (iii) Uandikishwaji rika lengwa la Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza unaongezeka kutoka asilimia 60 mwaka 2015 hadi asilimia 80 mwaka 2020.
- Kuhuisha taratibu za kujiunga na taasisi zinazotoa Elimu na Mafunzo katika ngazi mbalimbali kwa kutambua sifa zinazopatikana katika mifumo na Taasisi tofauti ili kuhakikisha kwamba:-
- Asilimia 20 ya wahitimu wa Elimumsingi wanaendelea na masomo katika ngazi za Sekondari ya Juu na asilimia 80 kuendelea na elimu au mafunzo ya ufundi katika ngazi ya cheti, stashahada au shahada kulingana na sifa, vipaji au vipawa;
- Asilimia 80 ya wahitimu wa Elimu ya Sekondari ya Juu kujiunga na Elimu ya Juu ya Taaluma na asilimia 20 kuendelea na Elimu ya Ufundi, katika ngazi ya cheti, stashahada au shahada kulingana na sifa; na
- (iii) Asilimia 70 ya wahitimu wa Elimu au Mafunzo ya Ufundi na Taaluma wanapata ajira kwa kujiajiri au kuajiriwa.
- Kudurusu na kuhuisha muundo wa mitaala ili elimu katika ngazi mbalimbali ikamilike kwa muda wenye tija na itilie maanani matokeo ya kusoma yenye kujenga ujuzi, maarifa ya kujitegemea, weledi na kuwawezesha wahitimu kumudu na kufanya kazi mbalimbali za kuajiriwa au kujiajiri;
- Kuhuisha vigezo na utaratibu wa kuhakiki, kusimamia na kupima utekelezaji wa mitaala katika shule na taasisi za elimu na mafunzo katika ngazi zote ili kuhakikisha kwamba:-
- Ufaulu wa mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi unaongezeka kutoka asilimia 57 mwaka 2015 hadi asilimia 90 mwaka 2020 na asilimia ya wanafunzi wanaoendelea na Kidato cha Kwanza kuongezeka kutoka asilimia 55.5 hadi asilimia 100;
- Ufaulu wa mtihani wa Kidato cha Nne unaongezeka kutoka wastani wa asilimia 69.8 mwaka 2015 hadi asilimia 90.0 mwaka 2020 na ufaulu wa daraja la I – III unaongezeka kutoka wastani wa asilimia 30.8 hadi asilimia 50.0; na
- Idadi ya wataalamu wenye ujuzi wa juu wanaongezeka kutoka asilimia 3 hadi asimilia 10 mwaka 2020, ujuzi wa kati kutoka asilimia 13 hadi 30 na ujuzi wa chini kupungua kutoka asilimia 84 hadi 60.
- Kuimarisha ithibati na udhibiti wa ubora wa Elimu na mafunzo ili kuhakikisha kwamba:
- Asilimia 60 ya wanafunzi wanahitimu shahada kwenye sekta ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi;
- Programu tatu (3) au zaidi za mafunzo zinaanzishwa zenye kukidhi mahitaji na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kulingana na mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa;
- Asilimia 70 ya wahitimu katika ngazi zote wawe katika mrengo wa sayansi, ufundi, hisabati na teknolojia;
- Kuandaa na kutumia utaratibu wa upatikanaji na usambazaji wa vitabu vya kiada na ziada kwa ngazi zote za Elimu na mafunzo ili kuhakikisha kwamba:-
- Uwiano wa kitabu cha kiada kwa mwanafunzi katika Elimumsingi unaongezeka kutoka 1:3 mwaka 2015 hadi 1:1 mwaka 2020;
- Asilimia 50 ya fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule zinatumika kuchapisha na kusambaza vitabu vya kiada; na
- Uwiano wa vitabu vya ziada kwa kila somo kwa mwanafunzi katika Elimumsingi kuwa 1:10.
- Kuandaa utaratibu, kuimarisha mfumo wa udahili na kutumia fursa za Elimu na Mafunzo ndani na nje ya nchi kwa makundi yote ya jamii kwa usawa katika ngazi zote hususan katika ufundi, hisabati, sayansi na teknolojia ili kuhakikisha kwamba:-
- Asilimia 100 ya wahitaji wa mikopo kwa ajili ya kusomea fani ya udaktari wanapata mikopo
- Ufadhili wa nafasi 500 za masomo ya fani ya udaktari zinapatikana kila mwaka ili kupunguza pengo la uhaba wa madaktari nchini;
- Asilimia 100 ya wale wenye mahitaji maalumu, vipaji na vipawa wataotambulika watapata fursa za kuendelea na masomo katika ngazi mbalimbali; na
- Shule moja maalumu ya Ufundi (Specialized Technical Schools) au zaidi inaanzishwa kila mkoa ambayo itadahili wanafunzi wenye vipaji mbalimbali na kuwaendeleza kwenye fani mbalimbali zenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
- Kuandaa mpango wa kuwawezesha walimu na wanafunzi kutumia TEHAMA katika kufundishia na kujifunzia ili kuhakikisha kwamba:-
- Asilimia 80 ya walimu wanaandaliwa na kutumia TEHAMA kufundishia katika ngazi zote; na
- Asilimia 70 ya taasisi zote zinazotoa elimu na mafunzo zinaunganishwa katika Mkongo wa Taifa
- Kuhuisha miongozo ya Elimu na Mafunzo ili kuondoa vikwazo vinavyosababisha mwanafunzi kushindwa kukamilisha mzunguko wa elimu au mafunzo ili kuhakikisha kwamba:-
- Mdondoko katika Elimumsingi unapungua kutoka wastani wa asilimia 2 mwaka 2015 hadi asilimia 2 mwaka 2020;
- Wasichana wote wa Elimumsingi wanaoacha shule kwa sababu ya kupata ujauzito wataendelea na masomo; na
- Wanafunzi wanaomaliza mzunguko wa elimu katika ngazi ya Elimumsingi wanaongezeka kutoka asilimia 67 mwaka 2015 hadi asilimia 95 mwaka 2020.
- Kuandaa walimu, wakufunzi na wahadhiri mahiri hususan katika masomo ya hisabati, lugha, sayansi, teknolojia na ufundi ili kuhakikisha kwamba:-
- Uondokaji wa walimu, wakufunzi na wahadhiri unapungua kutoka wastani wa asilimia 0.8 mwaka 2015 hadi asilimia 0.2 mwaka 2020;
- Tatizo la uhaba wa walimu wapato 24,000 wa masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za Sekondari linapungua kwa kutoa mafunzo kwa walimu 5,000 wa masomo hayo kila mwaka; na
- (iii) Idadi ya wahadhiri wanaongezeka kutoka wahadhiri 6,880 mwaka 2015 hadi wahadhiri 10,000 mwaka 2020.
- Kuandaa mpango kabambe wa kuongeza udahili katika taasisi za elimu na mafunzo kwa kuzingatia mahitaji ya rasilimali watu na ujuzi kwa maendeleo ya Taifa na soko la ajira hususan ujuzi unaohitajika au kuhusiana na sekta zinazokua haraka na zinazojitokeza mfano mafuta, gesi na madini ili kuhakikisha kwamba:-
- Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Sayansi Shirikishi cha Mwalimu J.K. Nyerere (Butiama) unakamilika na kuanzisha na kukamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Madini Shinyanga;
- Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Kagera utafanyika;
- Udahili katika vyuo vya Ufundi Stadi unaongezeka kutoka wastani wa wanafunzi 150,000 mwaka 2015 hadi wanafunzi 700,000 mwaka 2020;
- Udahili katika vyuo vya Ufundi vya Kati unaongezeka kutoka wastani wa wanafunzi 30,000 mwaka 2015 hadi wanafunzi 285,600 mwaka 2020; na
- Udahili katika ngazi ya shahada unaongezeka katika vyuo vya elimu ya Juu kutoka wastani wa wanafunzi 60,000 mwaka 2015 hadi wanafunzi 117,000 mwaka 2020.
- Kushirikiana na wadau katika kuimarisha mfumo wa ugharimiaji wa elimu ya mafunzo ikiwemo mikopo na ruzuku ili uwe endelelevu na wenye vyanzo anuai;
- Kuweka utaratibu wa ada na michango mbalimbali katika shule na vyuo binafsi ili kusimamia kwa ufanisi masuala ya ada na michango;
- Kuandaa utaratibu wa ushirikiano baina ya Sekta ya Umma, Binafsi na Jamii katika ugharamiaji wa maendeleo ya elimu na mafunzo katika ngazi zote ili kuhakikisha kwamba:-
- Mchango wa Sekta Binafsi katika kudahili wanafunzi katika vyuo vya Ufundi ngazi ya kati unaongezeka kutoka asilimia 21 mwaka 2015 hadi asilimia 25 mwaka 2020; na
- Mchango wa Sekta Binafsi kudahili wanafunzi katika ngazi ya shahada unaongezeka kutoka asilimia 35 mwaka 2015 hadi asilimia 40 mwaka 2020.
- Bajeti ya Sekta ya Elimu na Mafunzo inaongezeka kutoka asilimia 17.6 mwaka 2015 hadi asilimia 25 ya bajeti ya Serikali mwaka 2020;
- Bajeti ya Elimumsingi inaongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2015 hadi asilima 75 ya Bajeti ya Sekta ya Elimu na Mafunzo mwaka 2020;
- Bajeti ya Elimu ya Ufundi na Elimu ya Juu inaongezeka hadi kufikia asilimia 25 ya Bajeti ya Sekta ya Elimu na Mafunzo ifikapo mwaka 2020; na
- Kuendelea kusimamia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2015 ambayo inaifanya elimu ya Msingi hadi Sekondari kuwa ya lazima na bila ya malipo.
(o) Kuanzisha Tume ya Walimu itakayosimamia Maendeleo na Maslahi ya Walimu wote Nchini
Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17 – 2020/21
- Elimu ya awali, Msingi na Sekondari
(a) Kuimarisha mazingira ya utoaji wa Elimu katika ngazi zote,
(b) Kuimarisha utoaji wa Elimu Maalum,
(c) Kuboresha Mazingira ya wathibiti ubora wa shule;
(d) Kuhamasisha uchangiaji wa Elimu, sayansi na Teknolojia na Ubunifu katika ngazi zote;
(e) Kuhakikisha usawa unakuwepo katika usambazaji wa walimu katika ngazi ya wilaya;
(f) Kuhakikisha upatikanaji wa vifaa bora vya utafiti;
(g) Kuendelea kutekeleza Mpango Kambambe wa Elimumsingi bila malipo;
(h) Kuimarisha na kuongeza ufaulu katika masomo ya hesabu, sayansi na kiingereza katika ngazi zote za elimu;
(i) Kuhakikisha uwiano wa matokeo ya elimu na mahitaji halisi ya soko la ajira; na (j) Kuimarisha mafunzo elimu ya ualimu.
Vyuo vya Ufundi na Teknolojia
(a) Kukarabati na kupanua Miundombinu ya kufundisha na kujifunzia (madarasa, maabara, maktaba, hosteli);
(b) Kuongeza upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia; na
(c) Kujenga vyuo vya ufundi stadi kwa mikoa isiyokuwa navyo.
Elimu ya Juu
(a) Kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa;
(b) Kukarabati na kuongeza miundombinu ya kufundisha na kujifunzia;
(c) Kuongeza upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia;
(d) Kuimarisha miundombinu ya TEHAMA; na
(e) Kuimarisha utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu.
MAADHIMISHO YA SIKU ZA ELIMU
1-Siku ya Elimu Duniani- huadhimishwa mara moja kwa mwaka, kati ya (May- June kwenye wiki ya kwanza.
Lengo la siku hii ni kutambua mchango wa Walimu, Wazazi na Wanafunzi hasa katika ufaulu wa mtihani wa darasa la Saba na kidato cha Nne. Kupitia siku hii Waziri hutoa Tunzo kwa Wanafunzi 10 bora wa mtihani wa kidato cha Nne na Darasa la Saba.