JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU, WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU WIKI YA KUZUIA USUGU WA VIMELEA DHIDI YA DAWA ZA ANTIBIOTIKI
TAREHE 13- 19 NOVEMBA, 2017
- Wiki hii Dunia inaadhimisha wiki ya kupambana na Tatizo la Usugu wa Vimelea kwa Dawa za Antibiotiki (Antibiotics Resistance Awareness Week). Kauli mbiu ya mwaka huu wa wiki ya uhamasishaji kuhusu antibiotiki duniani unasema: “Fuata ushauri wa wataalam wa afya kabla ya kutumia antimicrobials”
- Dawa za Antibiotiki ni dawa ambazo zipo kwenye kundi kubwa linalojulikana kama antimicrobials. Antimicrobials ni dawa ambazo hutumika kuua au kuzuia ukuaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa ya kuambukiza kwa binadamu na wanyama.
- Tafiti za Kimataifa zinaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa duniani la matumizi ya dawa za antibiotikis’. Kwa mwaka 2000-2010 matumizi ya dawa za antibiotiki yaliongezeka kwa asilimia thelathini (30%). Pia, tafiti hizo zinaonesha kuwa kwa mwaka 2010 jumla ya tani 63,200 za antibiotiki zilitumika kwa mifugo peke yake.
- Dawa hizo zinatumika vibaya, ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 20- 50 ya antibiotiki zinatumika isivyo sahihi duniani.
- Hapa nchini Tanzania, Utafiti uliofanywa na Wizara mwaka 2014 katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya na Mwanza ilionesha matumizi makubwa ya dawa za antibiotiki hadi kufikia asilimia 67.7. Pia, tafiti zimebainisha kuongezeka kwa kiwango cha usugu wa antibiotikisi. Mfano, utafiti wa kitaifa uliofanyika juu ya usugu wa dawa za kifua kikuu (MDR-TB) ilionesha usugu wa dawa kwa wagonjwa wapya kuwa ni asilimia 1.1; na kwa wagonjwa wanaorudia dawa za TB baada ya kupona kuwa na usugu wa asilimia 3.9. Pia, katika kutibu ugonjwa wa malaria, usugu wa dawa za Chloroquine na Sulfadoxine/Pyrimethamine, au “SP” ulijitokeza na kupelekea kutumika kwa dawa ya sasa iitwayo Artemether/Lumefantrine, au “ALU”.
- Katika tafiti ya kutibu maambukizi ya njia ya mkojo (Urinary Tract Infection, au “UTI”) kwa kutumia dawa ya sindano ya gentamycin uliofanyika katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilionesha kuongezeka kwa usugu wa dawa hiyo kutoka asilimia 6.9 mwaka 2003 hadi asilimia 44 mwaka 2011. Aidha, katika kutibu ugonjwa huo, tafiti nyingine ilifanyika katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, ambapo imeripotiwa kuongezeka kwa usugu wa dawa ya sindano ya ceftriaxone kutoka asilimia 14 mwaka 2009 hadi asilimia 29.4 mwaka 2011.
- Zipo sababu nyingi zinazochangia uwepo wa usugu wa dawa za antimicrobials. Mojawapo ni maduka mengi ya dawa kuuza kwa wananchi dawa za antimicrobials bila cheti cha daktari au kutotoa dozi kamili. Ikumbukwe kuwa dawa za antimicrobials hutolewa kwa cheti cha daktari tu.
- Wakati mwingine dawa za binadamu hutumika kutibia wanyama kinyume na sheria za matumizi ya dawa. Pia wapo wafanyabiashara wanaoandaa vyakula vya wanyama ambao wamekuwa na tabia ya kuongeza antimicrobials kwenye vyakula hivyo kwa kufikiria kuwa zinasaidia mnyama husika kukua haraka na kutopata magonjwa.
- Madhara yanayoweza kutokea kutokana na usugu wa dawa za antimicrobials ni pamoja na magonjwa kushindikana kutibiwa na dawa hizo na hata kuweza kusababisha vifo.
- Matibabu mbadala baada ya dawa za kawaida kuwa sugu yanakuwa na gharama kubwa na ya muda mrefu. Mfano, matibabu ya mgonjwa mpya wa Kifua Kifuu kwa dawa za kawaida yanafanyika kwa kipindi cha miezi sita na yanagharimu takribani shilingi laki nne (400,000/=). Ikitokea mgonjwa huyo akapata kifua kikuu sugu matibabu hayo yanatibiwa kwa miezi 20 hadi 22 na gharama zake ni takribani shilingi milioni kumi na saba. Kama mgonjwa huyo atapata kifuu kikuu Sugu Zaidi matibabu yake yanakuwa ya muda mrefu zaidi na gharama kubwa takriban shilingi milioni 64.
- Watanzania wanashauriwa kuacha mazoea ya kununua dawa ovyo bila kupata cheti cha Daktari na ushauri wa wataalamu wa afya. Ndugu wananchi, vile vile nasisitiza ni muhimu sana kumaliza dozi za dawa.
- Kila mmoja wetu ana mchango mkubwa katika kuzuia uwezekano wa vimelea kujenga usugu dhidi ya dawa za antimicrobials. Mapambano dhidi ya usugu wa dawa za antimicrobials yatafanikiwa tu pale ambapo mimi na wewe kwa ujumla tutashiriki katika vita hii.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- AFYA
15 Novemba, 2017