Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Machi, 2019 amemuapisha Mhe. Valentino Mlowola kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Cuba.
Hafla ya kuapishwa kwa Mhe. Balozi Mlowola imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Prof. Adelardus Kilangi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Madhehebu ya Dini, Viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kumuapisha Mhe. Balozi Mlowola, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeamua kuanzisha Ubalozi wa Tanzania nchini Cuba kwa kutambua uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi hiyo ambao ulianzishwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, na pia kunufaika zaidi na fursa zilizopo nchini Cuba zikiwemo utalaamu na ujuzi wa uzalishaji wa miwa na sukari, uzalishaji wa dawa, ufundishaji wa madaktari,elimu na fursa nyingine.
“Nakupongeza kwa kukubaliwa na Cuba kuiwakilisha Tanzania katika nchi yao, sasa nataka ukafanye kazi, nataka tunufaike na Cuba ambao ni watalaamu wa kuzalisha miwa na sukari, waje wajenge viwanda vya sukari hapa Tanzania ili tukabiliane na upungufu wa sukari inayozalishwa hapa nchini” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Mlowola ameahidi kwenda kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuhakikisha malengo ya Mhe. Rais Magufuli pamoja na matarajio ya Watanzania yanafikiwa.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2017/18 iliyowasilishwa kwake na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna Diwani Athumani.
Katika taarifa hiyo Kamishna Diwani Athumani amesema TAKUKURU imepata mafanikio makubwa katika kuzuia na kupambana na rushwa katika mwaka 2017/18 na ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kuokoa fedha za Serikali kiasi cha shilingi Bilioni 70.3 ambazo zingepotea kutokana na vitendo vya rushwa,kurudisha shilingi Bilioni 13.1 zilizotokana na matukio ya ukwepaji wa kodi na kesi kubwa 3 za wakweji wa kodi ambazo kufunguliwa katika Mahakama Kuu kitengo cha rushwa na uhujumu uchumi zenye thamani ya shilingi Bilioni 27.7.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa kesi za rushwa zilizofunguliwa katika mahakama mbalimbali kutoka kesi 435 za mwaka 2016/17 hadi kesi 495 ambapo kati yake kesi 296 zimeamriwa na katika kesi 178 watuhumiwa wamepata adhabu ya vifungo mbalimbali, sawa na asilimia 60.1 ukilinganisha na asilimia 41 iliyofikiwa mwaka 2016/17.
Akizungumzia taarifa hiyo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na timu yake kwa juhudi kubwa wanazozionesha katika mapambano dhidi ya rushwa na ameitaka taasisi hiyo kuendelea kufichua mianya yote ya vitendo vya rushwa nchini.
Ametoa mfano wa mianya hiyo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa walipa kodi wenye mashine za kutolea risiti (EFD) zisizotambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), madai ya kughushiya marejesho ya kodi (Tax Refunds) na ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara akiwemo mfanyabiashara mmoja aliyekwepa kulipa zaidi ya shilingi Bilioni 8.3 kutokana na kuingiza nchini magari 176.
Mhe. Rais Magufuli pia amemtaka Kamishna Diwani Athumani kuhakikisha anawachukulia hatua wafanyakazi wa TAKUKURU ambao wanakiuka maadili ikiwemo kujihusisha na rushwa, akiwemo mtumishi mmoja ambaye anayedaiwa kujikusanyia zaidi ya shilingi Bilioni 1.4 kwa kuwauzia watumishi wa TAKUKURU viwanja hewa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika aliyeomba TAKUKURU isaidiwe kufungua ofisi katika wilaya mpya 21.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Machi, 2019