Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Jan 09, 2019
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 09 Januari, 2019 amewaapisha viongozi aliowateua jana pamoja na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma aliwateua hivi karibuni.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.

Walioapishwa ni Mhe. Doto Mashaka Biteko – Waziri wa Madini, Bi. Zainab Abdi Seraphine Chaula – Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Afya), Bi. Dorothy Aidani Mwaluko – Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera na Uwekezaji), Arch. Elius Asangalwise Mwakalinga – Katibu Mkuu Ujenzi, Bw. Faustine Rweshabura Kamuzora – Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Bi. Dorothy Onesphoro Gwajima – Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia afya na Dkt. Francis Kasabubu Michael – Naibu Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma walioapishwa ni Mwenyekiti wa Tume Mhe. Jaji Mstaafu Steven James Bwana, na Makamishna 6 ambao ni Bw.George Daniel Yambesi, Bw.Yahaya Fadhili Mbila, Bi. Hadija Ali Mohamed Mbarak, Bi. Immaculate Peter Ngwale, Bw. Daniel Ole Njoolay na Bw. John Michael Haule.

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kushika nyadhifa hizo na amewataka kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kutanguliza maslahi ya Watanzania wote.

Mhe. Rais Magufuli pia amewapongeza viongozi na watendaji mbalimbali wa Serikali na kueleza kuwa wanafanya kazi kubwa na nzuri huku akibainisha kuwa anatambua kuwa baadhi yao wanashindwa hata kwenda likizo kutokana na kukabiliwa na majukumu mazito ya kuwahudumia wananchi.

Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutorishwa na utendaji wa Wizara ya Madini hususani katika udhibiti wa utoroshaji wa madini na hivyo amemtaka Waziri aliyeteuliwa Mhe. Biteko na taasisi zilizo chini ya wizara yake kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na Benki Kuu ya Tanzania kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini ili kudhibiti utoroshaji na kuiwezesha Benki Kuu kuwa na hifadhi ya dhahabu.

“Tumewaruhusu wawekezaji na wachimbajiwadogo wachimbe dhahabu, Je Wizara ya Madini mmeshajiuliza dhahabu inayochimbwa inauzwa wapi? Na je kama wanachimba na wanauza sisi tunapata asilimia ngapi? Hili suala ni la Wizara ya Madini, halikuwa suala la Bunge kujiuliza, wala halikuwa suala la Waziri Mkuu au Rais kujiuliza.

“Kwenye sheria ya madini nina hakika kuna mahali imeelekeza kuanzishwa kwa vituo vya kuuzia madini, je vimeanzishwa vituo vingapi? viko wapi? Kwa sababu vingeanzishwa vituo hivi tungejua dhahabu inayosafirishwa, wapi imeuzwa  na inawezekana tungekuwa na taarifa za kila wiki, lakini hakuna” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro kwa kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi la Polisi kukamata zaidi ya kilogramu 300 za dhahabu Mkoani Mwanza na ametaka Askari Polisi 8 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa ukamataji wa dhahabu hiyo wachukuliwe hatua za kisheria.

Mhe. Rais Magufuli amewaonya viongozi wa Serikali ambao wamekuwa wakilumbana badala ya kufanya kazi na amesema vitendo hivyo vikiendelea hatasita kutengua uteuzi wao na kuteua viongozi wengine watakaofanya kazi bila malumbano.

Mapema wakitoa salamu, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamisi Juma wamewapongeza viongozi walioteuliwa na wamewataka kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, na kwamba Bunge na Mahakama zitatoa ushirikiano kwao.

Nae Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewapongeza viongozi walioteuliwa na kubainisha kuwa Serikali inaamini kuwa wataongeza nguvu katika utekelezaji wa ahadi ambazo imewaahidi wananchi hadi kufikia 2020.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

09 Januari, 2019

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi