Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Siri ya Uwanja wa Kassim Majaliwa na Ushindi wa Namungo FC
Jun 22, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_53441" align="aligncenter" width="750"] Wachezaji wa Namungo FC Wakifanya Mazoezi katika Uwanja wao wa Kassim Majaliwa Wilaya ya Ruangwa.[/caption]

Na Judith Mhina – Ruangwa

Ujenzi wa uwanja wa michezo wa Majaliwa umeleta hamasa kubwa na kufanya kila mkazi wa Ruangwa kushiriki kwa njia moja au nyingine katika kuhakikisha timu ya Halmashauri  ya Wilaya ya Ruangwa ( Namungo Football Club), inashinda kila inapokutana na timu za nje ya mkoa, katika uwanja huo.

Hii imedhihirika wazi pale wachezaji wa timu hiyo,(Namungo FC) wanapofanya mazoezi na uwanja kufurika watu utadhani wana mechi ya ligi kuu  ya Vodacom (Vodacom Primiers League). Idara ya Habari (MAELEZO), ilipata fursa ya kuongea na wasimamizi wa ujenzi wa uwanja huo, washabiki na wachezaji ambao walithibitisha kuwa uwanja huo umewaletea hamasa ya kuhakikisha kuwa wanashinda kila mechi.

Akihojiwa, mmoja wa washabiki wa Namungo FC, Mzee Hamza Hamisi amesema “Huu uwanja wa Kassim Majaliwa ni mwisho wa vigogo wote wa Ligi Kuu ya Vodacom, waulize wakwambie Simba na Yanga hawakuambulia kitu hapa, wametoka sare na timu yetu wengine tumewafunga, ila kiboko yetu ni Coastal Union ambao walitufunga bao tatu bila, siku ile sitaki kuikumbuka wana Ruangwa walihuzunika sana”, amesema

“Hapa Majaliwa Stadium wanapajua wote wanaocheza Ligi Kuu ya Vodacom, sisi Ruangwa tuna umoja kuanzia vijijini, vitongoji na mitaa, watu wote wanakuja kuishangilia timu yao, kila mmoja anashiriki kuweka mazingira ya timu yetu vizuri kwa hali na mali. Pia, mchango mkubwa na hamasa anayotoa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Ruangwa Mhe. Kassim Majaliwa ni chachu inayochangia Namungo  kufanikiwa ligi kuu na kushika nafasi ya nne”, ameongeza Mzee Hamisi.

Naye, Kocha Mkuu wa Namungo FC, Hitimana Thiery, amesema “Tunashukuru sana sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufungua michezo baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19), mimi na Meddie Kagere tulipewa kipaumbele kupitia kwa viongozi wa nchi zote mbili na kupata kibali cha kurudi Tanzania ili kushiriki katika maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom”.

Aidha, captain wa timu hiyo, Hamisi Mgunya amesema kuwa kwa dhati kabisa wanamshukuru Rais John Pombe Magufuli kufungua michezo hususan Ligi Kuu ya Vodacom na support kubwa wanayoipata kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  kwa kuwa haya ndio maisha yao ambapo ili uwe mchezaji mzuri na kupata ajira ni lazima kufanya mazoezi ya nguvu.

Kwa upande wake, mchezaji wa kimataifa wa Namungo FC, Bigirimana Blaise amesema “Mimi na wenzangu kama wachezaji wa Namungo FC kwa sasa mawazo yetu na fikra zote ni juu ya kupata ushindi Ligi Kuu, ni lazima tufanye jitihada za dhati kabisa kuhakikisha tunashinda mechi zote zinazotukabili, kama tunashindwa kuchukua ubingwa basi angalau kupata nafasi tatu za juu”.

“Ugonjwa wa Corona umeathiri kwa kiasi kikubwa michezo, binafsi kutokufanya mazoezi ya uhakika ninakuwa kama  mgonjwa  kwa hiyo kwangu, kufunguliwa kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania imenipa faraja na kunirejeshea uzima  wa mwili wangu, mazoezi magumu ni sehemu ya maisha yangu na  bila mazoezi siwezi kuwa mchezaji mzuri na hapo ndio mwanzo wa kukosa ajira, mimi mpira ndio kila kitu”, amesema Bigirimana

Naye mchezaji kutoka Bukina Faso Nurdin Abarora ameonyesha furaha yake ya kucheza mpira Tanzania na kusema, “Naona fahari kubwa kucheza Ligi ya Tanzania ambayo imenifanya mimi kufahamika sio tu Tanzania hata nchini kwangu kwa kuwa nacheza nje ya nchi. Ninachotaka kusema ni kuwa mimi, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa si  tu kama kiongozi bali ni baba yangu anayenilea na kunitunza kama mwanae kwa kweli namshukuru sana sana”

 Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Malugu Mwanganya amesema   “Kwa sasa ujenzi wa jukwaa kubwa unaendelea ambao unajumuisha vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji, vyumba vya marefarii, kumbi za mikutano, migahawa, ofisi mbalimbali, vyoo vya waamuzi, huduma ya kwanza, makamisaa wa michezo, chumba maalum (security room) na chumba cha wanahabari’.

Akielezea kazi ambazo zimefanyika awamu ya kwanza Mhandisi Mwanganya amesema kuwa ni pamoja na usafi wa eneo la mradi, kutengeneza eneo la kuchezea mpira wa miguu (pitch) kwa kuotesha nyasi, uchimbaji kisima kirefu (mita 67) pamoja na kuweka mfumo wa maji, utandazaji wa mfumo wa kumwagilia uwanja, ufyatuaji wa matofali pamoja na ujenzi wa uzio kuzunguka  uwanja na uwekaji wa mabango, mageiti matatu ya kuingia na kutoka, ujenzi wa uzio mdogo ndani ya uwanja, ujenzi wa vyoo na vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji ambao umekamilika kwa  asilimia 50 na ujenzi wa majukwaa ya kudumu ambao uko katika hatua za ujenzi wa nguzo.

Ujenzi wa uwanja wa Majaliwa unaendelea ambapo kwa sasa umefikia asilimia 56.2 na jumla ya shilingi milioni 758,938,936.58 zimekwishatumika hadi sasa. Uwanja huo ukikamilika utagharimu shilingi bilioni 1.2. Kukamilika kwake kutaleta hamasa ya mchezo wa mpira wa miguu mkoani Lindi na mikoa ya Kusini na utakuwa miongoni mwa viwanja bora na vya kisasa  nchini.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi