Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Shirika la Posta Kuanza Kupokea Maombi ya Fomu za Mikopo ya Wanafunzi Julai 8 Mwaka Huu
Jul 04, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu,

SHIRIKA la Posta Nchini (TPC) kupitia Ofisi zake 170 zilizopo nchini kuanzia Julai 8 mwaka huu litaanza kupokea na kusafirisha vifurushi vyenye fomu za maombi ya mikopo ya wanafunzi wa Juu nchini na kuziwasilisha katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Akizungumza leo Alhamisi (Julai 4, 2019) katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Meneja wa Usimamizi wa Fedha za Kigeni wa TPC, John Tinga alisema fomu zitasafirishwa zikiwa na bahasha maalum yenye nembo za HESLB na TPC.

Tinga alisema ili kurahisha zoezi hilo, TPC imeweka mawakala wake maalum watakaotumika kwa ajili ya kusaidia huduma za usafirishaji wa maombi hayo ikiwemo kutumia pikipiki katika maeneo yaliyopo sehemu za vijijini ili kuwezesha fomuhizo  kufika kwa urahisi katika ofisi za TPC zilizopo katika Ofisi zake za mikoa na Wilaya zote nchini.

Kwa mujibu wa Tinga alizitaja gharama za usafirishaji wa vifurushi hivyo ni Tsh 16,000 kwa fomu za maombi yatakayotumwa  kutoka mikoani ambayo yatawasilisha katika mfumo wa EMS wakati kwa upande wa DSM gharama za kutuma zitakuwa ni Tsh 8000 na hakutokuwa na gharama nyingine zozote zitakazotozwa kwa wateja hao.

Aliongeza kuwa TPC kwa kushirikiana na HESLB zimejipanga katika kuhakikisha kuwa zoezi hilo linaendeshwa kwa ufanisi mkubwa ili kuwawezesha wanafunzi wote nchini kuwasilisha maombi yao kwa wakati na kuepukana na usumbufu wa kutuma maombi hayo katika tarehe za mwisho.

“TPC imejipanga vizuri kwa ajili ya kufanikisha zoezi hili na hakuna fomu yoyote ya maombi itakayopotea tunachokihitaji ni kwa waombaji kukamilisha taratibu zote za msingi ikiwemo kuweka jina lake nyuma ya bahasha zetu” alisema Tinga.

Akifafanua zaidi Tinga alisema malengo ya Shirika hilo ni kutoa huduma bora kwa wananchi na wateja wote nchini ili kuhakikisha malengo ya Shirika hilo yanaweza kufikiwa ikiwemo kutoa huduma bora zinazozingatia viwango vya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Tinga alisema Shirika hilo pia limeanzisha huduma ya mfumo mpya wa mawasiliano wa ‘Net Smart’ inayowezesha kutuma na kupokea vifurushi vyote kwa njia ya haraka zaidi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi