[caption id="attachment_14102" align="aligncenter" width="750"] 5. Afisa Tathimini na Ufuatiaji wa Shirika la Pelum Tanzania, Frank Maimo akielezea kuhusu majukumu na kazi za shirika hilo, wakati wa mkutano baina yake na timu ya timu ya waandishi wa habari yaliyofanyika septemba 16, 2017 mkoani Morogoro.[/caption]
Na: Mwandishi Wetu,
SHIRIKA la Pelum Tanzania kupitia Mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika kusimamia Sekta ya Kilimo (CEGO) limepima na kutoa hati miliki za kimila za mashamba 4832 katika vijiji 30 vya Halmashauri 6 za Mikoa ya Iringa, Morogoro na Dodoma.
Hayo yamebainishwa jana Mkoani Morogoro na Afisa tathimini na Ufuatiliaji wa PELUM Tanzania, Frank Maimo wakati wa semina elekezi ya kuwajengea uwezo Viongozi wa Vijiji na wananchi wakiwemo Wakulima na Wafugaji kuhusu Mpango wa Matumizi ya Ardhi Vijijini.
Maimo anasema PELUM Tanzania imekusudia kuhakikisha kuwa maeneo yaliyoanishwa katika mradi huo yanaondokana na changamoto za umiliki wa ardhi ikiwemo migogoro ya mara kwa mara na kuhakikisha kuwa CEGO inaongeza fursa za uwekezaji katika kilimo na sekta nyingine.
Anasema ili kufanikisha makusudio ya mradi huo, PELUM imekuwa ikishirikiana kwa karibu zaidi na Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya kuweza kuendesha mafunzo mbalimbali na kuwezesha upatikanaji wa vibali vya hati za umiliki.
“Kupitia Mpango wa matumizi bora ya ardhi tumekusudia kuhakikisha kuwa wananchi tunapima mashamba ya wananchi 5000 na kuwapatia hati miliki za kimila, ambapo kwa kufanya hivi migogoro baina ya wakulima itakuwa historia”
Anaongeza kuwa hadi sasa, mradi wa CEGO umewezesha kuundwa kwa kamati katika vijiji 25 ambavyo vimeweza kusimamia na kutoa maamuzi na mashauri ya kesi mbalimbali zitokanazo na migogoro ya ardhi.
Akifananua zaidi anasema mradi wa CEGO umekusudia kuwajengea uwezo Wakulima na Wafugaji kuweza kutambua umuhimu wa matumizi ya ardhi ikiwemo kufanya kilimo endelevu na kinachokidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na baadaye bila kuathiri ardhi na mazingira” anasema Sensia.
Kwa upande wake, Afisa Mipango Miji na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Andrea Biashara anasema Mradi wa CEGO umekuja katika wakati mwafaka kwa kuzingatia migogoro ardhi ikihusisha mipaka na mashamba imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya jamii ya Wakulima na Wafugaji.
Anaongeza kuwa Serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa itasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo ili uweze kuleta tija iliyokusudiwa ikiwemo utoaji wa hati za ardhi za mashamba na mipaka ya viijiji vya Wakulima na Wafugaji ili kuachana na mfumo usio rasmi wa umiliki wa ardhi.
Anasema katika Mkoa wa Morogoro, mradi wa CEGO unatekeleza katika Halmashauri za Wilaya ya Mvomero na Morogoro Vijijini kwa kuwa maeneo hayo ndiyo yenye idadi kubwa ya jamii za Wakulima na Wafugaji, hivyo Serikali itahakikisha kuwa jamii zinaondiokana na migogoro ya umiliki wa inayojitokeza mara kwa mara baina yao.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni, Wilayani Mvomero, Stephano Udoba alipongeza juhudi za PELUM Tanzania kwani semina hiyo imewapa mwanga wa matumaini ya umoja na mshikamano baina ya jamii za Wakulima na Wafugaji katika Wilaya hiyo.
“Katika kipindi cha nyuma, eneo letu lilikuwa na migogoro wa ardhi isiyo na usuluhishi baina ya wakulima ya wafugaji, hivyo kupitia msaada wa PELUM Tanzania katika upimaji wa mashamba na mipaka ni wazi sasa kesi za wananchi kufikishana Mahakamani zitapungua” anasema.
Mradi wa CEGO unaotekelezwa katika Halmashauri na Mikoa ya Iringa (Kilolo, Mufindi), Dodoma (Bahi, Kongwa), na Morogoro (Mvomero, Morogoro Vijijini) umeanza Disemba 2013 na unatarajia kukamilika Desemba 2017.