[caption id="attachment_43475" align="aligncenter" width="750"] Moja ya Kifaa cha kampuni inayojenga Reli ya Kisasa, SGR ya Yapi Merkez kikiunganishaji Reli hiyo katika moja ya zaiara ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Makataibu tawala takribani 400, Mei 14, 2019.[/caption]
Na. Paschal Dotto
Ni Takribani Miaka 120 ambapo historia iliandikwa, mwaka 1912, Serikali ya Kikoloni nchini iliamua kuimarisha sekta ya usafirishaji Kwa kujenga Reli, ambapo njia zake ziliunganisha Miji hasa maeneo ya kilimo, uzalishaji na kibiashara, reli kuu kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, hatimaye Kigoma na Tanga.
Ni dhahiri sasa tunaona Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akifanya mageuzi makubwa Kwa kujenga reli ya kisasa, maarufu SGR (Standard Gauge Railway) ambapo kwa vyovyote tutasogeza nyuma zaidi kuhusu historia ya reli nchini, kwani Rais anatakeleza Ujenzi wa Reli ya Kisasa, Standard Gauge Railway (SGR) kwa maslahi makubwa kiuchumi.
Katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya SGR awamu ya pili, Morogoro-Makutupola, iliyofanyika 14, Machi, 2018, Rais Magufuli aliwakumbusha Watanzania kuwa Tanzania imekuwa nchi ya pekee Barani Afrika katika kutekeleza mradi huo mkubwa kwa pesa za walipa kodi wake.
“Kwa bahati nzuri, hivi karibuni tulitembelewa na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, na alishuhudia kwamba Tanzania tumetayarisha fedha zetu wenyewe, kwa nguvu zetu wenyewe, na walipa kodi ni watanzania wenyewe, Tsh Trilioni 2.8 na kutangaza tenda zilizokuwa wazi, makampuni zaidi ya 40 yalijitokeza kuwania tenda, na bahati nzuri kampuni kutoka Uturuki ikashinda tenda hii,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa Uturuki itatupa mkopo wa masharti nafuu kwa awamu zingine za ujenzi, Rais akaongeza, “ kwa hiyo Tanzania tunaweza”,
Rais Magufuli aliwataka watanzania kutambua fursa za upitapo mradi wa SGR na kuwataka wafanyabiashara wakubwa, wadogowadogo, mama ntilie, kunufaika wakati wa ujenzi na mara baada ya ujenzi, na kwamba itakuwa nguzo kubwa kwa usafarishaji kwenye maeneo hayo na nchi nzima.
“Katika uchumi wa nchi yoyote duniani, Sekta ya Usafirishaji ni muhimu sana, kwa hiyo Serikali kuchukua hatua madhubuti ya kuimarisha sekta ya usafirishaji kwa kujenga reli ya kisasa, SGR, ni moja ya Mwarobaini wa kutatua changamoto ya usafirishaji mizigo na kulinda usalama wa barabara”. Alisikika mmoja wa wahandisi akiwaeleza waliowatembelea.
[caption id="attachment_43476" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya Watalaam wanaoshirika ujenzi wa Reli ya Kisasa, SGR kutoka Tanzania na Kampuni ya Ujenzi ya Yapi Merkezi wakishuhudia zoezi la uunganishwaji wa reli ya Kisasa katika ziara ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Makataibu tawala takribani 400, Mei 14, 2019.[/caption]Mageuzi ya Rais Magufuli yanalenga kuwaimarisha wananchi, si tu wafanyabiashara bali hata wasafiri kwa utekelezaji wa ujenzi wa Reli ya kisasa, SGR yenye kasi ya 160km/saa utakuwa na faida kuwabwa kwani masaa 2.5 Dar es Salaam-Morogoro na masaa tisa kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, ni dhahiri kutakuwa na Furaha kubwa kwa watu kuwahi kufika Mwanza mapema badala ya saa saba usiku au kulala Shinyanga.
“Ujenzi wa Reli hii (SGR), kwa Tanzania siyo chaguo bali ni lazima, kwani hatua hii ilitakiwa ifikiwe zamani, lakini sasa Rais Magufuli ameamua kutufikisha kwenye teknolojia mpya katika sekta ya usafirishaji, kwani matatizo mengi ya barabara yanatokea kwababu ya mizigo mizito, hakuna reli imara ya kubeba mizigo hiyo, kwa hiyo ujenzi wa Reli hii ni maamuzi sahihi kwa Serikali yetu.”, Anaeleza Mkurugenzi TRC, Masanja Kadogosa.
Kadogosa anasema, Reli hiyo ambayo inatumia nishati ya umeme imekuja wakati mwafaka ikiwa Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Mto Rufiji (Rufiji Hydroelectric Power), wenye kutoa Megawati 2,115, kwa hiyo treni hiyo itapata umeme wa kutosha.
“SGR, Ni mradi mkubwa ambao unatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufulu kwa kutumia fedha za walipa kodi wake kwahiyo ni vyema watu wakafahamu kuwa kodi yao inaenda wapi Trilioni 7 siyo mchezo”, alisema Kadogosa.
Ili kutekeleza adhima ya kuutangaza mradi huo kwa wananchi, Mei 17, 2019, Jopo la Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Makatibu Tawala takribani 400 wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Seleman Jafo walitembelea kuona mradi huo ili kupeleka ujumbe kwa wananchi.
Kabla ya Safari hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa aliwapitisha kidogo wageni wake katika shule ndogo kuhusu mradi ili kutambua umuhimu wa Mradi huo kwenye sekta ya usafirishaji na kwa wananchi.
Masanja alieleza kuwa Reli hiyo inayojengwa inaenda kufuta zana mbalimbaliikiwemo ile historia ya kikoloni, kuwa reli iliyopo ilijengwa na wakoloni, lakini pia ujenzi wa Reli hiyo sasa unaenda kuimarisha sekta ya usafirishaji.
Serikali inatekeleza ujenzi huo Kwa Kipande cha Dar es Salaam-Morogoro, Morogoro-Makutupola na badae kutekeleza ujenzi huo hadi Mwanza, kilometa 1,219.
Kadogosa alisema kuwa Reli hiyo, SGR inauwezo wa kubeba tani milioni, 10,000, kwa mkupuo sawa na malori 500 yenye tani 20, Treni tano zenye tani 10,000 na kuwa na kasi kubwa ya 160km/saa, tofauti na ya sasa ambayo inakasi ya 30km/saa, kwa Afrika itakuwa ni Reli pekee yenye uwezo mkubwa kama huo, tani Miliomi 10-17 zitasafirishwa kwa mwaka, kwa hiyo SGR ni mwamba sekta ya usafirishaji nchini.
Aidha, Kadogosa alieleza kuwa ujenzi wa Reli (SGR), Dar es Salaam-Morogoro unatekelezwa na Kampuni kutoka Uturuki, Yapi Merkezi takribani Trilioni 2.7, lakini kwa sehemu nyingine ni Yapi Merkezi na Portuguese Construction Group Motel-Engil.
kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na ufanisi mkubwa kwenye sekta ya usafirishaji nchini kwa kubeba mizigo tani nyingi lakini pia kasi yake katika kusafirisha abiria, kutoka Dar es Salaam- Dodoma treni itakuwa inafanya safari mara nane kwa siku, kwa hiyo ni hatua kubwa kwa sekta ya usafirishaji.
Kadogosa alizitaja baadhi ya Faida za Mradi huo Kwa sasa kwa wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla kwani kwa sasa watanzania walioko sehemu za ujenzi wanafaidika na kupeleka malighafi za ujenzi, mama ntilie kupika chakula na biashara zingine,
“Takribani mifuko ya simenti milioni, 9,200,000 ambayo ni sawa na tani 600, nondo kilo milioni 115 sawa na tani 1500 na mataluma 1,400,000, kutoka kwa wasambazaji wa malighafi hizo takribani 500, wafanyakazi 10, 000, huku asilimia 94 ya wafanyakzi hao ni watanzania, pia asilimia 48 ya wataalam ni watanzania, kwa hiyo pamoja na mradi huu kuwa nguzo imara ya usafirishaji nchini, SGR imekuja kutoa Fursa za ajira kwa watanzania”, Alisema Kadogosa.
Kadogosa alisema kuwa mradi huo ni mkubwa na uwezo wake ni wa juu, na sasa matatizo ya usafarishaji nchini yatapata suluhu kubwa, kuimarisha na kulinda barabara nchini.
Katika sekta ya usafirishaji wa mizigo hasa ile mikubwa inayotoka bandarini kwenda sehemu zingine za nchi na mengine nje ya nchi, kwani kuwepo kwa Reli imara itasababisha utendaji kazi wa bandari kuwa na ufanisi mkubwa, “Bandari inategemea kuwepo kwa miundombinu imara kwa upande wa nchi kavu, hakuna ufanisi wa Bandari bila kuwa na Reli imara, Serikali imeliona hilo ndiyo maana ikaamua kutekeleza haraka ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Reli yetu hii inabeba mizigo mingi Takribani Tani Milioni 17 kwa mwaka, hakuna Reli kama hii Barani Afrika” Kadogosa.