Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa hatua mbalimbali zilizofikiwa katika kuendeleza sekta hizo, akisema kuwa kilimo, mifugo na uvuvi ni miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa na maendeleo ya viwanda.
Rais Samia ameyasema hayo Agosti 8, 2026, jijini Dodoma, wakati akishiriki kilele cha Sherehe za Nanenane Kitaifa, ambapo pia amepongeza maandalizi na maonyesho yaliyofanyika katika maonesho hayo.

“Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuhakikisha wananchi, hususan wakulima na wafugaji, wanapata tija na kunufaika moja kwa moja na shughuli zao,” amesema Rais Samia.
Amewapongeza vijana kwa ubunifu wao katika sekta ya kilimo, akiwemo kijana aliyeonesha ubunifu wa ndege nyuki kwa ajili ya kusaidia katika shughuli za kilimo.
Pia, Rais Samia amekubali kutoa mtaji kwa kijana huyo ili aweze kutengeneza ndege nyingine zitakazosaidia wakulima katika shughuli mbalimbali, ikiwemo upuliziaji wa dawa shambani.
Sambamba na hayo, amelipongeza Shirika la AGRA kwa mchango wake katika kuendeleza sekta ya kilimo, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mbinu na taaluma zinazozalishwa na wataalamu zinawafikia wakulima kwa wakati.

“Mbinu na taaluma zimfikie mkulima ili mkulima, mvuvi na mfugaji anufaike, ili tupate matokeo ya moja kwa moja,” amesisitiza Rais Samia.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Bashilu Ally Kakuru, amesema kuwa Serikali imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya mifugo na uvuvi kupitia ongezeko la bajeti ya Wizara hiyo.
Ameendelea kusema bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeongezeka kutoka Sh168.25 bilioni mwaka 2022/23 hadi kufikia Sh433.38 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Ambapo ongezeko hilo limewezesha Serikali kuongeza nguvu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mifugo na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo, na kufanya kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa thamani na idadi ya mifugo nchini, sambamba na kuongezeka kwa miradi inayolenga kuimarisha sekta hiyo.