Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yawapa Watanzania Nafuu Tozo za Miamala
Sep 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Paschal Dotto-MAELEZO

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amsema kwamba Serikali imezingatia maoni ya wananchi kwa kufanya marekebisho katika tozo licha ya kwamba tozo hizo zilianzishwa ili kukidhi mahitaji ya bajeti.

Akizungumza Bungeni leo Septemba 20, 2022, Waziri, Mwigulu amesema kuwa uamuzi wa kuanzishwa kwa tozo hizo ilikuwa ni busara ya kiuchumi iliyotaka sekta zingine za uzalishaji upelekewe fedha nyingi ili kuimarisha upatikanaji wa ajira kwa vijana.

“Tulipoamua kuanzisha tozo lilikuwa suala la busara ya kiuchumi ambalo lililenga kuimarisha sekta za uzalishaji huku sekta za huduma za kijamii zikihudumiwa na tozo za miamala ya kifedha, Serikali ilitenga Shilingi bilioni 143 ujenzi wa vituo vya afya kati ya hizo, Shilingi bilioni 117 zilikuwa ni tozo ya miamala, Shilingi bilioni 611.3 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kati ya hizo Shilingi bilioni 221.3 zilikuwa za miamala ya kifedha”, ameeleza Dkt. Mwigulu.

Dkt. Mwigulu amesema kuwa katika kutatua shida ya ubovu wa barabara vijijini, Serikali ilitenga bilioni 735 ambapo kati ya hizo bilioni 13.5 zilitokana na miamala ya kifedha na zilihakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kupita katika barabara zilizoboreshwa.

Dkt. Mwigulu pia ameeleza kuwa uwepo wa tozo za miamala ya kifedha uliwezesha kutengwa kwa bilioni 954 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na mbegu bora katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji ambayo inawapa vijana ajira ili kutatua tatizo la ajira nchini.

“Serikali ilitumia busara ya kiuchumi kupeleka fedha shilingi bilioni 954 kwenye kilimo, bilioni 147 kwenye mifugo pamoja na wamachinga, biloni 150 kwenye ruzuku ya mbolea kwa wakulima na hii inatokana na kuimarisha uzalishaji wa chakula ili kupunguza mfumuko wa bei kwenye vyakula”, amesema Dkt. Mwigulu.

Waziri Mwigulu amesema kuwa katika kutekeleza majukumu ya kuimarisha Elimu na Afya nchini, bilioni 500 ambazo zilitokana na tozo za miamala ya kifedha zilitumika kujenga madarasa 8,000 kati ya madarasa 17,000 hitajika, kujenga vyuo 72 vya VETA katika Wilaya ambazo hazikuwa na vyuo hivyo, kutekeleza mpango wa elimu bila malipo kwa kidato cha tano na sita pamoja na kujenga Vituo vya Afya pamoja na ununuzi wa vifaa tiba katika maeneo ambayo hayakuwa na huduma hizo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi