Na; Frank Mvungi
Serikali imewakikishia wanachi kuwa azma ya kuwapatia huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85 kwa maeneo ya Vijijini na asilimia 95 kwa wananchi waishio mijini ifikapo 2020.
Akijibu swali la mbunge wa viti maalum Mhe. Maria Ndilla Kangoye, Naibu Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso amesema kuwa dhamira hiyo inaendelea kutekelezwa ambapo utekelezaji wake kwa upande wa vijijini kupitia program ndogo ya Huduma ya Maji Vijijini na usafi wa Mazingira.
“Kufikia mwezi Septemba, 2018 jumla ya miradi 1,595 imekamilika, Serikali inaendelea kukamilisha miradi inayoendelea na kupanua miradi iliyopo na kuanzisha miradi mipya ili kufikia lengo lake la kuwapatia huduma wananchi wote”; Alisisitiza Mhe Aweso
Akifafanua amesema kuwa kwa upande wa miradi ya mijini, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji inayohusu ujenzi na ukarabati katika Miji Mikuu ya Mikoa, Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo pamoja na miradi ya Kitaifa ambapo miradi yote ipo katika hatua za mbalimbali za utekelezaji.
Aliongeza kuwa Bwawa la Kidunda ambalo litasaidia kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam yamekamilika ikiwa ni pamoja na usanifu,nyaraka za zabuni, michoro pamoja na ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa bwawa hilo.
“ Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo zinazokadiriwa kufikia shilingi bilioni 470”;Alisisitiza Mhe. Aweso
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji hapa nchini ikiwemo kutekeleza miradi ya kimkakati.