Na Abubakari Akida, MOHA
Serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuunganisha kambi za wakimbizi kwa kuanza na kambi za Nduta na Mtendeli ambapo kambi ya Mtendeli inafungwa na wakimbizi wote waliopo Kambi ya Mtendeli kuhamishiwa Kambi ya Nduta.
Hayo yamebainika leo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo kutembelea Kambi za Nduta, Mtendeli na Nyarugusu zilizopo mkoani Kigoma.
Akisoma taarifa ya uendeshaji wa shughuli za wakimbizi mbele ya Naibu Waziri, Kaimu Mratibu wa Wakimbizi Kanda ya Kigoma, Kuyega Matenya alisema baada ya kukamilika kwa zoezi hilo katika Kambi ya Mtendeli wanatarajia pia zoezi hilo kuhamia Kambi ya Nyarugusu.
“Zoezi hili limeanza tarehe 26 Julai mwaka huu na hadi kufikia leo (5 Agosti) ambapo jumla ya watu 1,253 walikuwa wamekwisha ondoka na zoezi hili ni endelevu huku kila juma kutakuwa na misafara mitatu ya kuhamisha watu kutoka Mtendeli kwenda Nduta”, alisema Kuyega.
Akizungumzia hali ya urejeaji amani katika nchi ya Burundi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo amesema amani imerejea nchini humo na kumekua na ziara za mara kwa mara kwenda nchini Burundi kati ya Serikali na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) lengo kukagua urejeaji wa amani na shughuli za kimaendeleo nchini humo.
“Sisi Tanzania tumekua na historia ya muda mrefu ya kupokea wakimbizi na kuwahifadhi lakini sasa umefika muda wakimbizi kurejea katika nchi zao kwa hiyari baada ya amani kurejea, ni vizuri sasa walio tayari wajiandikishe kurudi nyumbani na niwahakikishie amani imerejea katika nchi zao sisi serikali tumekua tukituma wajumbe wetu kwenda kuhakikisha kama kweli amani imerejea Burundi na ni kweli tumethibitisha kurejea kwa amani nchini Burundi”, alisema Naibu Waziri Chilo
Jumla ya wakimbizi na waomba hifadhi walioko kwenye kambi za wakimbizi ni 171,098 na wakimbizi wa mwaka 1972 ni 49,234, makazi ya zamani ni 27.726 na wakazi wa Kigoma vijijini ni 21,508 ambapo jumla kuu ni 220.332 huku serikali ikiwa na mpango wa kuwarejesha katika nchi zao za asili baada ya kurejea kwa amani.