Serikali imeonya kuwa haitakuwa na msalie mtume na mtu, Chama cha Siasa ama kikundi chochote kitakachojihusisha na rushwa kabla,wakati na baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu 2019 pamoja na Uchaguzi mkuu wa 2020.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi wakati akifungua mkutano wa kujadili namna ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 jijini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli inataka wananchi watambue kuwa serikali yao imedhamiria kupambana na rushwa katika nyakati zake zote na sura zake zote.
“Sote tunafahamu mwaka 2019 tutakuwa na uchaguzi katika ngazi za Serikali za Mitaa hivyo basi,chaguzi hizi zinapaswa kuendeshwa na kusimamiwa kwa uadilifu na umakini mkubwa kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu ili haki,usawa,uhuru na demokrasia viweze kustawi,kuendelezwa na kudumishwa hivyo Takukuru kamwe isiwe na Msalie Mtume kwa yeyote atakayejihusisha na masuala ya rushwa”, alisema Prof. Kabudi.
Profesa Palamagamba John Kabudi ameongeza kuwa rushwa katika uchaguzi ni zaidi ya udanganyifu wa hesabu za kura, kwa kuwa una madhara kadha wa kadha ikiwemo viongozi kukosa uwajibikaji, kukosa viongozi waadilifu, kukosa viongozi wazalendo, uwepo wa vitendo vya uvunjifu wa Amani kutokana na migogoro ya mara kwa mara ya kisiasa,uchumi wa Taifa kudidimia kwa kukosa mipango ya maendeleo na viongozi kufanya maamuzi ya kisera yenye maslahi kwa wachache.
Aidha, amewapongeza TAKUKURU kwa kuandaa Warsha hiyo katika wakati muafaka na kusisitiza, pamoja na sheria na kanuni zilizopo bado kuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha jamii inashirikishwa na kuelimishwa kuhusu madhara ya rushwa katika Uchaguzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini TAKUKURU Kamishna wa Polisi Diwani Athumani amesema rushwa katika Uchaguzi ni hatari na inaweza kuleta madhara kwa Taifa kwani viongozi wala rushwa au watoa rushwa hawataweza kuisimamia nchi kwa misingi ya haki,usawa,uwazi,uwajibikaji na uzalendo na vilevile wananchi wapokea au watoa rushwa hawawezi kuhoji masuala mbalimbali kwa viongozi wao.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha na kutoa taarifa bila woga kwa wale wote watakaojihusiha na masuala ya utoaji ama upokeaji rushwa ili sheria ziweze kufuata mkondo wake na baadae kuwa na Taifa lenye usawa katika nyanja zote.
Warsha hiyo ya wadau kujadili namna ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa imehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wadini,vyama vya siasa,vyama vya kiraia na vyombo vya ulinzi na usalama.