[caption id="attachment_42404" align="aligncenter" width="688"] Viongozi wa Wizara ya Nishati na Shirika la umeme Tanesco wakionesha mfano wa hundi ya malipo yenye thamani ya Dola za Kimarekani zaidi ya milioni 309 ambazo ni zaidi ya Shilingi bilioni 688 yalitolewa kwa mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa Kufua Umeme wa Maji Bonde la Mto Rufiji leo Jijini Dar-es-salaa. Kuanzia kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamis Mwinyimvua, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Dkt. Tito Mwinuka na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco, Dkt. Alexander Kyaruzi.[/caption]
Na.Paschal Dotto-MAELEZO.
Serikali imekabidhi hundi yenye thamani ya Tsh. bilioni 688.651 kwa Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa mradi wa kufua umeme Mto Rufiji (Arab Contructors) na kuwahakikishia wajenzi jinsi serikali ilivyojipanga katika kutekeleza mradi huo na nia ya serikali kuimarisha sekta ya nishati nchini.
Katika makabidhiano hayo, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema kuwa kukabidhiwa kwa kiasi hicho kikubwa kwenye mradi wa maendeleo ni kwa mara ya kwanza kufanyika nchini katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
“Serikali imeweza kuzilipa Tsh.bilioni 688.651 kwa mkupuo, jambo ambalo halijawahi tokea kwa malipo ya awali kwenye miradi, kwani miradi mingi ya maendeleo huwa inaishia kwenye Tsh.bilioni 50 au kiasi kikubwa kabisa Tsh.bilioni 100, kwa hiyo ukizungumzia bilioni 688.651 kama malipo ya awali kwenye mradi ni kiasi kikubwa sana”, Katibu Mkuu, James.
Aidha James alisema kuwa katika kukamilisha mradi huo wa kufua umeme mto Rufiji kutawezesha kupatikana kwa megawati 2,115 kutoka kwenye chanzo hicho ambacho ujenzi wake unaendelea kutekelezwa na kampuni ya ujenzi ya Arab Contructors kutoka Misri.
James aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo mkubwa nchini kutaleta faida nyingi kwa wananchi ikiwemo, kuwepo kwa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya viwanda na maendeleo ya wananchi kwa ujumla, kuwepo kwa bei nafuu ya umeme nchini pamoja na kutoa ajira zisizo za kudumu kati ya 4000-6000.
“ni matumaini yangu kuwa mkandarasi atafanya kazi usiku na mchana ili kuweza kukamilisha mradi ndani ya mkataba wa miezi 36, kwani katika malipo ya awali ya asilimia 15 ya mradi mzima, kiasi kilichotoka leo ni asilimia 70 ya malipo ya awali na mkandarasi ameishakamisha asilimia 30 ya mkataba, ambapo pia atalipwa malipo yaliyobaki kwenye malipo ya awali, ili wananchi waweze kufurahia huduma itokanayo na mradi huu”, ameahidi Katibu Mkuu.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamis Mwinyimvua amesema kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuweza kutekeleza mradi huo mkubwa na kwamba Mkandarasi achape kazi akijua pesa zipo.
“kiasi kilicholipwa kama alivyoeleza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ni asilimia 70 ya fedha za malipo ya awali ambayo ni asilimia 15, nichukue nafasi hii kumhakikishia mkandarasi asiwe na wasiwasi fedha zipo, na leo tumewahakikishia kuwa fedha zipo kwa hiyo mradi huu hautateteleka kamwe katika ujenzi wake”, Katibu Mkuu, Mwinyimvua.
Mnamo Disemba 12, 2018 jijini Dar es Salaam, Serikali ilisaini Mkataba wa ujenzi wa Mradi wa kufua umeme, Mto Rufiji baina yake na kampuni ya ujenzi Arab Contructors kutoka Misri wenye thamani ya Tsh.Trilioni 6.5, kujenga mtambo utakaofua umeme wa Megawati 2,115 pindi utakapokamilika miaka mitatu ijayo.