Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yajipanga Kutokomeza Mmea Aina ya Gugu Karoti Katika Hifadhi Za Wanyamapori.  
Dec 07, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Mwandishi Wetu,Arusha.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema  Serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa mmea  hatari uitwao gugu karoti hauoti katika maeneo ya hifadhi  kwa kuwa una madhara makubwa kwenye malisho ya wanyamapori .

Amesema mmea huo ukiota ndani ya maeneo ya hifadhi umekuwa ukizuia uoto asili kuota na hivyo kupelekea kutoweka kwa malisho ya wanyamapori.

Amesema mmea huo ulibainika miaka tisa iliyopita na umekuwaa ukisambaa katika maeneo ya nje ya  hifadhi  na athari zake zimekuwa zikionekana wazi wazi.

Amesema baada ya matokeo ya utafiti kuhusiana na mmea huo, Serikali imeamua kuiongezea bajeti   Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI)  ili  iweze kufanya tafiti zaidi kuhusiana na mmea huo.

‘’Serikali kupitia Wizara yangu tumejipanga kuhakikisha kuwa mmea huo unatokomezwa kabisa.’’ Alisisitiza  Hasunga.

Alibainisha hayo leo mjini Arusha katika Mkutano wa  utafiti wa kisayansi uliowakutanisha Wanasayansi 300  waliofanya tafiti mbalimbali katika hifadhi za wanyamapori  na mazingira kwa ujumla wa   kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Mkutano huo umeanza leo na utafanyika kwa muda wa siku tatu ambapo wanasayansi watafiti mbalimbali wataziwasilisha na kuzijadili tafiti zao zipatazo 167 katika maeneo hayo.

Aidha, Naibu Waziri Hasunga amesema mkutano huo utatoa nafasi ya kubadilishana uzoefu, mawazo na pia ni fursa ya kutangaza vivutio vya utalii tulivyonavyo kwa wanasayansi hao.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAWIRI, Prof.  Aporinalia Pereka amesema kwa upande wa Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) nao tayari wameanza kufanyia utafiti  mmea huo ili usiweze kusambaa zaidi kwa kuwa una madhara kwa wanyamapori na kwa binadamu pia.

Amesema kwa upande wa binadamu mmea huo umekuwa na madhara katika ngozi na upande wa wanyamapori umekuwa ukiathiri uoto asili na hivyo kupelekea  malisho ya wanyamapori kutoweka.

Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo wa Bodi,Prof. Pereka ameiomba serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii iendelee kutenga bajeti ya kutosha ili  Taasisi hiyo iweze kufanya tafiti nyingi zaidi katika maeneo mengi ya nchi tofauti na sasa inavyofanya.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi