Serikali kupitia Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika kipindi cha miaka miwili, imetoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya vifaa baada ya kuanzisha huduma mpya, kufufua na kuziimarisha kwa kufanywa na Watalaamu Mabingwa nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Prof. Abel Makubi alisema kuwa wagonjwa 31 wa huduma ya kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua wamefanyiwa upasuaji ambapo gharama za upasuaji huo nchini ni kati ya shilingi milioni 8 hadi 16 na nje ya nchi ni zaidi ya shilingi milioni 40.
Alitaja huduma zingine zilizoanzishwa na Taasisi hiyo kuwa ni, huduma ya matibabu ya maumivu sugu ya mgongo bila ya upasuaji ambapo tangu kuanza kwa huduma hiyo mwezi Mei 2023 tayari wagonjwa 97 wamepata huduma hiyo na gharama za upasuaji huo nchini ni shilingi milioni 1 na nje ya nchi ni zaidi ya shilingi milioni 9.
Sambamba na kufufuliwa kwa huduma za upasuaji marudio ya vipandakizi ambapo wagonjwa 57 wa kurekebisha nyonga na magoti kati ya wagonjwa ambao walifanyiwa upasuaji katika kipindi cha miaka 15 hadi 19 iliyopita.
“Huduma hizi mpya, zimeiwezesha Taasisi kupunguza kero nyingi za ucheleweshaji wa matibabu na hata wagonjwa wengine kupata madhara ya kudumu lakini pia zimepunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa nje ya nchi ambapo kwa sasa kwa magonjwa ya ubongo na mishipa ya fahamu asilimia 96 tunafanya hapa na upasuaji wa mifupa asilimia 98 tunafanya hapa”, alibainisha Prof. Makubi.
Halikadhalika, Prof. Makubi alisema kuwa katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa kisasa huduma za maabara ya upasuaji wa ubongo zimeendelea ambapo katika kipindi cha miaka miwili wagonjwa 276 wamehudumiwa na gharama za huduma hiyo nchini ni shilingi milioni 5 hadi 10 na nje ya nchi ni milioni 30 hadi 60.
“Katika kuimarisha ubora wa huduma za uchunguzi katika Taasisi ya MOI, Serikali imetoa shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya ununuzi wa mashine mpya ya kisasa ya MRI na CT scan kwa lengo la kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma hiyo kwa uhakika na wakati bila ya kusubiri muda mrefu na kurahisisha ugunduzi wa magonjwa”. Alifafanua Prof. Makubi.