Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akionesha mkoba wenye hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021
Jonas Kamaleki, Dodoma
Serikali imefuta tozo 173 ambazo zilikuwa kero kwa wananchi ili kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Hayo yamesemwa leo Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Isidor Mpango wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2020/2012.
“Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (The government Roadmap for Improvement of Business and Investment Climate) na Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blue Print for regulatory Reform to Improve Business Environment) kwa lengo la kuhakikisha vikwazo na kero mbalimbali za biashara na uwekezaji zinaondolewa ili kuvutia uwekezaji zaidi nchini”, amesema Dkt. Mpango.
Kwa mujibu wa Dkt. Mpango utekelezaji wa programu hizo umewezesha kufutwa kwa takribani tozo 114 katika Sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa mwaka 2017/2018, kufutwa kwa tozo tano (5) zilizokuwa zinatozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi(OSHA), na tozo 54 katika sekta mbalimbali mwaka 2018/19 ikiwemo kuanzishwa kwa vituo vya utoaji huduma kwa pamoja mpakani (One Stop Border Posts-OSBPs)katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani ambavyo vimeimarisha biashara baina ya Tanzania na nchi jirani.
Aidha, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (zamani ikiitwa Mamlaka ya Chakula na Dawa) ambazo zilikuwa na majukumu yanayoingiliana. Utekelezaji wa hatua hizo umewezesha mazingira ya biashara nchini kuimarika. Na hii imedhihirishwa na Taarifa ya Benki ya Dunia ya Wepesi wa Kufanya Biashara (Ease of Doing Business Report) ya mwaka 2020 inayoonesha Tanzania imepanda kwa nafasi 3 kufikia nafasi ya 141 kutoka nafasi ya 144 mwaka 2019.
Serikali imeanisha mapendekezo ya hatua mpya za viwango vya Ushuru wa Forodha ikiwemo kupunguza Ushuru wa Forodha hadi asilimia 0 kutoka viwango vya awali vya asilimia 10 na asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa vifaa maalum vinavyotumika katika kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID19) vikiwemo Barakoa (Masks), kipukusi (Sanitizer), mashine za kusaidia kupumua (ventilators), na mavazi maalum ya kujikinga yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya (PPE).
“Msamaha huu utatolewa kwa utaratibu wa “duty remission”. Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa uzalishaji wa vifaa hivyo hapa nchini ili kuongeza kasi katika kupambana na ugonjwa huo, kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Cash registers, Electronic Fiscal Device (EFD) Machines and Point of Sale (POS) na kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vinavyotumiwa na wazalishaji wa maziwa kwa joto la juuyanayodumu kwa muda mrefu (UHT Milk)”, amesisitiza Dkt. Mpango
Waziri Mpango ameomba Bunge liidhinishe bajeti ya jumla ya Shilingi trilioni 34.88 kwa matumizi ya maendeleo na kawaida kwa Mwaka wa Fedha 2020/21.