Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yafanyia Utafiti Mbadala wa Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo
Aug 22, 2023
Serikali Yafanyia Utafiti Mbadala wa Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis (mwenye kaunda ya bluu) akiwasilisha taarifa ya hatua zilizofikiwa juu ya uratibu na utekelezaji wa Mpango-kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki (2020 - 2025) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo tarehe 22 Agosti, 2023. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama.
Na Robert Hokororo

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imefanya utafiti kuhusu teknolojia mbadala wa zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini. 

Amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya hatua zilizofikiwa juu ya uratibu na utekelezaji wa Mpango-kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki (2020 - 2025) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira. 

Kwa mujibu wa Mhe. Khamis, utafiti umeonesha teknolojia za kuchoma (smelting) kwa kutumia borax na teknolojia za sianadi (cyanidation) ndio zinatumika kwa wingi nchini na nchi zinazoendelea.

Amesema Mradi wa Kudhibiti Athari za Zebaki kwa Afya ya Binadamu na Mazingira Kwenye Shughuli za Uchimbaji Mdogo wa Dhahabu Nchini umejikita katika kufanyia kazi teknolojia zinazotumika zaidi nchini. 

 

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwa katika kikao cha kupokea taarifa ya hatua zilizofikiwa juu ya uratibu na utekelezaji wa Mpango-kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki (2020 - 2025) iliyowasilishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dodoma leo tarehe 22 Agosti, 2023.

”Lengo ni kutekeleza malengo ya Mkataba wa Minamata hususan kipengele cha saba kinachohusu kupunguza matumizi ya zebaki kwenye uzalishaji wa dhahabu inayozalishwa na wachimbaji wadogo na pale itakapowezekana kuondoa kabisa matumizi ya kemikali hiyo katika kuzalisha dhahabu kwa wachimbaji wadogo,” alifafanua.

Pia, Naibu Waziri Khamis alitaja shughuli za mradi kuwa ni kuimarisha na kujenga uwezo na ujuzi wa taasisi na wachimbaji wadogo kuhusu namna ya kudhibiti athari zinazotokana na utumiaji wa zebaki kwenye uzalishaji wa dhahabu.

Aidha, katika kutekeleza Mpangokazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeandaa Mwongozo wa Uingizaji, Matumizi na Utupaji Salama wa Zebaki.

Mhe. Khamis amesema kuwa Mwongozo huo unalenga kutoa utaratibu wa njia salama za usimamizi wa Zebaki pasipo kuathiri afya ya binadamu na mazingira. 

Mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na Global Environmetal Facility (GEF) kwa ruzuku ya Dola za Marekani 7,339,450 sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 18.3. Unatekelezwa katika mikoa saba ya Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga, Singida, Mbeya na Songwe. 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi