Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Sasa Kuziunganisha RAHCO na TRL
Sep 14, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu

Serikali imewatoa hofu watumishi wote wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) na Shirika la Reli Tanzania (TRL),  kwa kuwahakikishia kuwa ajira zao hazitaathirika kwa kuwa sheria mpya ya Reli ya Mwaka 2017 imeweka utaratibu maalum kwa watumishi hao kuhamia kwenye taasisi mpya ya Kampuni ya Reli  Tanzania (TRC).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho amesema hayo katika mahojiano maalum mjini Dodoma na kusisitiza taratibu zote za kiutumishi zitafuatwa kwa watumishi watakoendelea na kazi kwenye kampuni mpya.

"Sheria mpya ya reli mwaka 2017 imezigatia maslahi ya watumishi kwa kuweka mazingira mazuri kwa wafanyakzi  wa RAHCO na TRL hivyo atakaetaka kuendelea kutumikia umma katika shirika hili jipya ataendelea na kazi na atakaetaka kuacha kazi basi taratibu za kiutumishi zitafuatwa kwa mujibu wa taratibu na Kanuni" alisema Dkt. Chamuriho.

Dkt. Chamuriho amesema kuwa lengo la kuunganisha taasisi hizo ni kuongeza ufanisi wa shirika hasa kwenye usaifirishaji wa mizigo na kuondoa tofauti zilizokuepo kati ya RAHCO na TRL ambazo zimekuepo kwa muda mrefu kwenye usimamizi na uendeshaji wa shirika hilo.

Kwa upande wa Reli ya Kisasa (SGR) Dkt. Chamuriho amesema kuanzishwa kwa sheria mpya kutaongeza ufanisi wa utekelezaji wa mradi huo kwa awamu ya kwanza ambayo inahusisha awamu tano ambapo awamu ya kwanza itajengwa kuanzia Dar es Salaam- Morogoro, Awamu ya pili Morogoro-Makutupora, awamu ya tatu Makutupora-Tabora, awamu ya nne Tabora-Isaka na awamu ya tano ni Isaka-Mwanza.

Aidha ameongeza kuwa baada ya awamu hizo kukamilika Serikali itaanza awamu ya pili itakayohusisha sehemu za Tabora-Kigoma, Mpanda-Kaliua na Ruvu-Tanga-Moshi-Arusha.

Kupitishwa kwa Sheria ya Reli ya mwaka 2017 na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunaifuta sheria ya Reli No. 4 ya mwaka 2002 na sheria hii itaanza kutumika baada ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuisaini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi