Na Immaculate Makilika–MAELEZO
Serikali imesema itakapofika siku ya mwisho wa mwezi Mei mwaka huu itakuwa ni mwisho wa kutumia mifuko ya plastiki nchini.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuwa akitoa majumuisho ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Ifikapo tarehe 30 Mei mwaka huu itakuwa ni mwisho wa kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa mbalimbali” alisema mheshimiwa Majaliwa.
Mbali ya kusitisha matumizi ya mifuko hiyo inayolaumiwa kwa kuongeza kasi ya uharibifu wa mazingira, Waziri Mkuu Majaliwa aliongeza kuwa kuanzia Juni mosi itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuagiza au kuuza mifuko hiyo.
Waziri Mkuu amesema lengo la serikali la kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo ni kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na mioundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki.
Matumizi ya plastiki nchini yameendelea kuleta madhara makubwa yakiwemo vifo vya mifugo kwa kula plastiki, kuziba mifereji mingi nchini na uchafuzi wa mazingira.
Kuhusu viwanda na sekta zinazotumia vifungashio vya plastiki kama vile kilimo na afya, Waziri Mkuu Majaliwa amelieleza bunge kuwa havitaathirika na katazo hilo hadi hapo serikali itakapotoa mwongozo.