[caption id="attachment_42350" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akijibu swali wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni leo.[/caption]
Na: Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha pembejeo za kilimo (mbegu, mbolea, viuatilifu na zana za kilimo) zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu.
Hatua hizo ni pamoja na uagizaji wa pamoja, ruzuku, kufuta au kupunguza tozo na kodi zinazochangia kuongezeka kwa bei ya pembejeo na kufanya tafiti katika mnyororo wa thamani wa mazao.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 24 Aprili 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ndanda Mhe Cecil David Mwambe aliyetaka kufahamu kwanini Pembejeo za kilimo ni ghali sana, hivyo wakulima wengi hushindwa kununua na kusababisha kupata mavuno haba na kama Serikali ipo tayari kupunguza au kuweka bei elekezi iliyo nafuu kwa mkulima ili aweze kupata pembejeo za madawa, mbolea na zana za kilimo.
Alisema kuwa Serikali ina utaratibu wa kuweka bei elekezi ya mbolea kupitia Mfumo wa Ununuzi wa pamoja nchini kwa mbolea za kupandia aina ya DAP na kukuzia aina ya Urea. Utaratibu huu unalenga kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu.
Mhe Mgumba aliongeza kuwa katika jitihada za kuongeza uzalishaji na kipato cha mkulima, Serikali hununua na kusimamia uthibiti na usambazaji wa viuatilifu vya kupambana na milipuko ya visumbufu vya mazao na mimea kama vile kweleakwelea, viwavijeshi, viwavijeshi vamizi, panya, nzige wekundu na nzi wa matunda.
Kadhalika, ili kumpunguzia mkulima harubu katika uzalishaji na uongezaji thamani ya mazao, Serikali imeendelea kutoa mikopo nafuu ya zana za kilimo kupitia Mfuko wa Taifa wa Pambejeo za Kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Shirika la Maendeleo la Taifa.
Kwa upande wa mbegu na viuatilifu, Mhe Mgumba alisema kuwaserikali inafanya utafiti wa kubaini gharama za uzalishaji wa mbegu kwa kulinganisha na bei za mbegu zilizopo sasa ambao utaiwezesha Serikali kuamua endapo kuna ulazima wa kuweka bei elekezi.
Aidha, Mhe Mgumba pamoja na hatua hizo, Serikali inahamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea, viuatilifu, zana za kilimo na uwekezaji katika mashamba ya mbegu ili kupunguza gharama za pembejeo hizo.