Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuongeza Nguvu kwa Walemavu Kushiriki Mashindano ya Kimataifa
Sep 01, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma

Serikali inakusudia kuwasaidia zaidi wanamichezo wenye ulemavu kushiriki katika michezo mbalimbali kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na vifaa vya michezo na watalaam wa michezo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul Agosti 31, 2021 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali namba 1626 alilouliza Mhe. Mwatatu Mbaraka Khamis ambaye alihoji Je, Serikali ina mpango gani wa kuwainua watu wenye Ulemavu kwa kuwapatia vifaa vya michezo na walimu ili waweze kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa?

“Kwa mwaka 2021, Serikali imelipia usafiri, vifaa na posho kwa wachezaji na viongozi wanne kushiriki michezo ya Paralimpiki inayofanyika Tokyo Japan, kuanzia Agosti 24 hadi Septemba 04, 2021.” Amesema Mhe. Gekul.

Katika kufanikisha mashindano hayo ya kimataifa, mwaka 2021, Serikali pia iliigharamia timu ya riadha kwa ajili kushiriki mashindano ya kufuzu kwenda kwenye Paralimpiki yaliofanyikia nchini Dubai.

Naibu Waziri Gekul amesema ili kusimamia sekta ya maendeleo ya michezo kwa weledi, Serikali imetengeneza Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Michezo wa Taifa ambao utazinduliwa rasmi Septemba 2021.

Mpango mkakati huo una malengo ya kuendeleza michezo kwa ujumla wake ikiwa ni pamoja na michezo ya watu wenye ulemevu ambao una ainisha maeneo yote muhimu yakiwemo upatikanaji wa vifaa, ujenzi na ukarabati wa miundombinu, uendelezaji na upatakinaji wa watalaam na walimu wa michezo.

Katika kufanikisha michezo nchini, mwaka 2019, Serikali iligharamia timu ya mchezo wa ‘wheel Chair’ kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki Nairobi Kenya pamoja na timu ya taifa ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu kushiriki mashindano ya Bara la Afrika (CANAF) yaliofanyika nchini Angola ambayo imefuzu kushiriki mashindano ya dunia ya mchezo huo yatakatofanyika mwaka 2022 nchini Uturuki.

Aidha, Naibu Waziri Gekul ameongeza kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ambao upo chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) utaendelea kuwasaidia wachezaji wenye ulemavu kwa mahitaji mbalimbali ili waweze kushiriki kikamilifu katika michezo ya kitaifa na kimataifa kwa kuwapata maandalizi na kuwa na vifaa bora na watalaam wa kuwafundisha.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi