Fedha za ziada kuwepo katika mzunguko wa uchumi sio kigezo cha kukua kwa uchumi wa Taifa bali ni ishara ya Taifa hilo kushindwa kudhibiti ukuaji wa uchumi wake.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Konde Mhe. Khatib Said Haji, aliyehoji kuhusu dhana ya kukua kwa uchumi nchini ilihali kuna upungufu wa uuzaji bidhaa nje na wananchi kukosa fedha.
Dkt. Kijaji alieleza kuwa matatizo ya kuwepo kwa fedha za ziada katika uchumi ni makubwa, hivyo inapongezwa hatua ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kudhibiti hali hiyo kwa manufaa ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Uchumi wa Tanzania unakua kutokana na hali halisi na takwimu zilizopo, ambapo katika Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) uliofanyika hivi karibuni ulieleza kuwa nchi nyingi mwanachama wa Jumuiya hiyo hazijafanikiwa katika ukuaji wa viashiria vya uchumi mkubwa isipokuwa nchi ya Botswana, Lesotho na Tanzania”. Alieleza Dkt. Kijaji.
Akijibu swali la Msingi la Mbunge huyo kuhusu vigezo vinavyoainisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania, Dkt. Kijaji alisema kuwa vigezo kwa mujibu wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa ni ongezeko la pato la Taifa, ongezeko la pato la wastani la mwananchi kwa mwaka na ongezeko la uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi.
Vigezo vingine ni kupungua kwa uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, utulivu wa bei za bidhaa na huduma, utulivu wa viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni, kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni na kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo na huduma za kijamii.
Vilevile alieleza kuwa, uwekezaji unaofanyika katika nchi ni kigezo cha msingi cha ukuaji wa uchumi kwa kuwa huongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa na huduma, ajira, kipato cha mwananchi mmoja mmoja na pato la Taifa hivyo kupunguza umaskini katika jamii.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji alibainisha kuwa, mchango wa Serikali katika ukuaji wa uchumi ni pamoja na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuwekeza zaidi kwenye shughuli zinazochochea ukuaji wa uchumi, kupunguza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji wa bidhaa na huduma nchini.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango.