Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali kujenga Kituo Dar cha Kukusanya na Kuuza Maziwa
Aug 24, 2017
Na Msemaji Mkuu

Meneja masoko wa bodi ya maziwa Tanzania (TDB) Dkt. Mayasa Simba akieleza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani ) katika ukumbi wa Idara ya Habari –MAELEZO Jijini  Dar es Salaam kuhusu ujenzi wa soko la maziwa la Ubungo Dar es Salaam, kushoto ni Meneja Idara ya huduma ya maziwa wa bodi hiyo Bw. Deogratius Mlay.

Na Paschal Dotto- MAELEZO

Serikali kupitia Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) inatarajia kujenga kituo cha kukusanya na kuuza maziwa Jijini Dar es Salaam ili maziwa yanayozalishwa kutoka maeneo mbalimbali ya jiji hilo yaweze kupatikana sehemu maalum ambapo wanunuaji watafika kwa urahisi.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Meneja Masoko wa Bodi ya Maziwa Dkt. Mayasa Simba amesema lengo la kujenga kituo hicho ni kudhibiti ubora na usalama wa maziwa kwa mlaji na tayari Manispaa ya Ubungo imekubali kutoa eneo la kujenga kituo hicho ambacho kitagharimu fedha za kitanzania shilingi bilioni 1.4.

“Kituo hicho kitajengwa Ubungo kwa sababu zaidi ya lita  6,000 hadi 10,000 huuzwa katika eneo hilo ambako wachuuzi wengi hufanya kazi zao, kwa hiyo tumeona  kuna haja ya kujenga kituo ili kuwe na sehamu nzuri ya upatikanaji wa maziwa bora na salama kwa watumiaji” alisema Dkt. Mayasa.

Dkt. Mayasa alieleza kuwa wachuuzi hao huuza maziwa katika maeneo ya kituo cha mafuta kilichopo Ubungo Mataa, Riverside na Ubungo External Barabara ya Mabibo Hostel hivyo si rahisi kwa wanunuzi wa bidhaa hiyo kuipata kwa muda lakini kukiwa na eneo maalum kutawezesha biashara yao kuthaminika na kupata faida kubwa.

Meneja wa Idara ya huduma ya maziwa wa bodi ya maziwa Tanzania Bw. Deogratius Mlay (kulia) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu ujenzi wa soko hilo pamoja na takwimu za matumizi ya maziwa. Katikati ni Meneja Masoko wa Bodi hiyo Dkt. Mayasa Simba na kushoto ni Afisa Habari wa Bodi hiyo Bi.Queenter Mawinde.

Aliongeza kuwa wateja takribani 700 hadi 800 hufika kwenye maeneo hayo kila siku kununua maziwa ambapo bei yake ni kuanzia shilingi 1,000 hadi 1,500 kwa lita.

Akiendelea kutaja faida za kituo hicho Dkt. Mayasa alisema kuwa kitasaidia kudhibiti uuzaji holela wa maziwa kwenye chupa za plastiki zilizokwishatumika ambazo si salama kiafya.

Alibainisha kuwa kituo hiki pia kitasaidia Bodi hiyo kuratibu Sheria na Kanuni za Maziwa kote nchini ikiwemo kurahisisha ukusanyaji wa tozo za maziwa (Milk Cess) na kuboresha sekta ya maziwa pamoja na kutoa ushindani kwa soko la maziwa Afrika Mashariki.

Katika Mpango wa Miaka Mitano ulioanza 2013/2014 mkakati wa Bodi ni kuhakikisha kwamba wadau wa tasnia ya maziwa wanafuata Sheria ya Maziwa na kuhakikisaha kuwa bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora.

“Zao lenyewe ni nyeti kwa hiyo litahitaji umakini mkubwa sana kwani likiandaliwa vibaya linaweza kuleta madhara makubwa sana kwa watumiaji”, alisisitiza Dkt. Mayasa.

Naye Meneja Idara ya Huduma ya Maziwa Bw. Deogratius Mlay alisema kuwa katika takwimu zilizopo, mwaka huu watumiaji wa bidhaa hiyo kwa maana ya walaji wameongezeka kutoka asilimia 45 mwaka 2016 mpaka asilimia 47 mwaka 2017, huku asilimia 70 ni maziwa ya ng’ombe wa kienyeji na 30 ni wa kisasa na asilimia 10 tu ya maziwa yote ndio inaenda sokoni.

Kwa upande mwingine Bodi ya Maziwa imetoa tahadhari kwa wananchi wote kuepuka kununua maziwa yaliyohifadhiwa au kuuzwa kwenye chupa za maji za plastiki kwa kuwa chupa hizo si salama kutokana na wauzaji kuziokota ovyo mitaani kisha kuwekea maziwa.

Aidha Bodi hiyo imewaomba wahisani na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kusaidia ujenzi wa kituo hicho kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya maziwa na uimarishaji wa afya ya watanzania.

(Picha Na Paschal Dotto-MAELEZO)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi