Adeladius Makwega -WHUSM –Dodoma.
Serikali inaanza zoezi la kukusanya nyaraka zote za utafiti wa kiutamaduni na kuzihifadhi kigitali kwani imeonekana wazi nyaraka zote zilizohifadhiwa kwa mfumo wa zamani zinaweza kuharibika na kupotea kabisa kama zoezi hilo lisipofanyika kwa haraka.
Akizungumzia zoezi hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Mnata Resani amesema kuwa mara baada ya Serikali kuhamia Dodoma mwaka 2017 baadhi ya nyaraka muhimu zilibaki Dar es Salaam na maeneo mengine kwa hiyo ili ziweze kutumika na kuweza kupatikana kwa urahisi ni lazima zihamishiwe katika kwenye mfumo wa kigitali.
“Zisipofanyiwa hivyo zinaharibika kwa haraka, zikiharibika siyo rahisi kupatikana tena, maktaba hai inayotoa simulizi hizo haipo tena kwani watu wa namna hiyo wengi wao wamefariki.” Aliongeza Dkt.Mnata.
Alibainisha kuwa mara zoezi hilo litakapomalizika basi kutapatikana takwimu sahihi za tafiti na kumbukumbu muhimu zitakazotumika kuhuisha Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 na rejea za wadau wa utamaduni.
Nyaraka hizo zitawekwa kwenye tovuti ya Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo (www. Habari.go.tz) na mitandao ya kijamii ili kila anayetaka aweze kupata taarifa hizo.
Wizara na Taifa kwa ujumla kuwa na kumbukumbu nzuri ambazo zilileta mchango mkubwa katika mageuzi ya Sekta ya Utamaduni.
Wakingumzia zoezi hili baadhi ya maafisa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wamesema kuwa zoezi hili linamanufaa makubwa kwa Watanzania haswa wa kizazi cha sasa.
“Mimi kwa umri wangu mambo mengi ya zamani ziyafahamau lakini kwa kusoma tafiti hizo naweza kujifunza mengi na kuweza kujua pa kuanzia kwani kwa kuzisoma tafiti hizo nitajua pale waliopofikia wenzetu na mimi kufanya tafifi zingine na bora zaidi.” Alisema Bi Hadija Kisubi ambaye ni Afisa Utamaduni.
Aliongeza kuwa zoezi hilo pia litasaidia sana kuokoa muda wa kutafuta tafiti hizo na kujua kwa haraka kilichomo kwa kutumia mitandao ya kisasa na siyo kwenye makabati.
“Unajua tafiti hizo zilifanyika na Serikali ilitumia mamilioni ya fedha kwa hiyo kama nyaraka hizo zitaharibika au kupotea hiyo itakuwa hasara kubwa kwa taifa letu, ndiyo maana tunafanya zoezi hilo.” Aliongeza Ombeni Mbesere ambaye ni Afisa Utamaduni wa wizara hii.