Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuendelea Kutoa Fedha za Bajeti kwa Miradi ya Maendeleo
Sep 15, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Beatrice Lyimo- Dodoma

Serikali imesema itaendelea kutoa fedha zaidi za Bajeti kulingana na ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ile inayopewa kipaumbele.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati akiahirisha Mkutano wa Nane wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mjini Dodoma.

“Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2017/2018 na mwenendo wa utekelezaji wake unaridhisha. Serikali imeweka jitihada kubwa za kuimarisha ukusanyaji mapato ya ndani kwa kutumia mifumo ya kielektroniki”, amefafanua Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Agosti, 2017 Serikali imetoa jumla ya Shilingi Trilion 3.944 zinazotokana na mapato ya ndani na fedha za nje kwa matumizi ya Serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ulipaji wa mishahara ya watumishi wa umma na kulipia deni la Taifa.

Aidha, Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa Serikali itahakikisha kila kituo cha kutolea huduma za afya nchini kinakuwa na vifaa vya kutosha ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeendelea kuimarika” ameongeza Mhe. Majaliwa.

Akizungumzia suala la elimu, Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea na mpango wa Elimu bila malipo kwa kupeleka fedha moja kwa moja katika shule za Umma za Msingi na Sekondari nchi nzima.

Kwa upande wa Kilimo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeamua kuanza kwa kuweka mkazo wa kuyaendeleza kwa kasi mazao makuu matano ya biashara yakiwemo Pamba, Tumbaku, Korosho, Chai na Kahawa.

Waziri Mkuu ameahirisha rasmi Bunge la Jamburi ya Muungano wa Tanzania mpaka mwezi Novemba mwaka huu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi