Serikali imesema kuwa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania ikiwemo kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji kutoka nje.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga, aliyetaka kujua mikakati ya Serikali kuongeza thamani ya Shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na nchi jirani za Afrika Mashariki.
Mhe. Nchemba alisema Serikali inaendelea kulinda thamani ya shilingi nchini ikiwa ni pamoja na shughulikia tatizo la upungufu wa dola ili kuweza kukabiliana na changamoto inayoendelea kutokea duniani.
Alisema miongoni mwa hatua zinachukuliwa na Serikali ni pamoja na kushirikisha Sekta Binafsi katika kuimarisha mikakati ya kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi pamoja na kuhimiza wananchi kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini ili kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni.
“Kuendelea kusimamia utekelezaji wa kifungu 7(3) na 13(1) cha Kanuni za Fedha za Kigeni za mwaka 2022, zinazoelekeza wafanyabiashara kuweka katika benki zilizopo nchini fedha za mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ndani ya siku 90 tangu siku ya kusafirisha bidhaa au kutoa huduma na wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje kufanya malipo kwa kutumia benki na taasisi nyingine za fedha zilizopo nchini”, alibainisha Mhe. Nchemba kuwa ni miongoni mwa hatua za kunusuru thamani ya shilingi nchini.
Alisema Serikali pia itaendelea kusimamia kwa karibu wazalishaji wa ndani ili kuongeza ubora katika uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa lengo la kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Waziri huyo alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu na kusimamia utekelezaji wa sera ya fedha ili kuhakikisha utulivu wa mfumuko wa bei nchini.
Wakati huo huo, Mhe. Nchemba amelieleza Bunge kuwa hesabu zinazowasilishwa na Maafisa Masuuli wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka ni za uhakika kwa kuwa zinaandaliwa na kuwasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 30 (2) cha Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348, viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma (IPSAS), miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na mifumo madhubuti ya kielektroniki ya usimamizi wa fedha ikijumuisha Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE).
Dkt. Nchemba alieleza hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde Mhe. Mohammed Said Issa, aliyetaka kujua uhakika wa hesabu zinazowasilishwa na CAG kila mwaka.
Aidha alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2019/20 – 2021/22), taarifa ya CAG imeonesha ongezeko la hati zinazoridhisha kutoka asilimia 92 mpaka 96 kwa Serikali Kuu, asilimia 70 mpaka 94 kwa Serikali za Mitaa, na kutoka asilimia 97 mpaka 98 kwa mashirika na taasisi nyingine za umma.