Na Mwandishi Wetu Mwanza
Serikali kupitia Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kuanzisha Vituo vya Malezi na Makuzi ya awali kwa watoto wenye umri kati ya miaka mitatu na minne nchi nzima, ikiwa ni moja ya mikakati ya kumjenga na kumlinda mtoto.
Kauli hii imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu alipofanya ziara katika kituo cha malezi na makuzi ya awali ya mtoto cha Nyerere kilichoko Igombe Ilemela jijini Mwanza.
Dkt. Jingu amesema Vituo vya malezi na Makuzi kwa watoto ni muhimu ili kuhakikisha wanapata huduma bora zitakazowezesha uchechemuzi wa bongo zao kuwekwa katika mazingira mazuri ya ukuaji.
“Hivi ni vituo muhimu unaweza ukadhani ni jambo dogo, hili ni jambo kubwa sana na la msingi katika malezi na makuzi kwa watoto wetu” alisema Dkt. Jingu.
Ameongeza kuwa vituo hivyo vitakuwa suluhisho tosha kwa tatizo la malezi na makuzi ya mtoto hasa kwa changamoto za utafutaji kipato kwa wazazi kukosa muda mwingi wa asubuhi mpaka jioni kukaa na watoto wao.
“Vituo vya malezi na makuzi ya awali kwa watoto vinalenga kutoa fursa kwa wazazi na walezi kutekeleza shughuli za kiuchumi”, aliongeza.
Naye Afisa Mradi Kituo cha Malezi na Makuzi cha Nyerere, Julieth Joseph amesema kuwa Kituo cha Malezi na Makuzi ya Mtoto cha Nyerere kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2016 mpaka mwaka 2019 kimefanikiwa kuwaandaa watoto zaidi ya 400 kabla ya kuwapeleka katika shule za awali.
“Walimu katika shule tulizowapeleka watoto hao wanasema watoto wanaopatia katika kituo hiki wanakuwa na uelewa wa haraka ukilinganishwa na watoto amabao hawajapitia katika vituo vya malezi”, alisisitiza
Ameongeza kuwa ujifunzaji kwa watoto umezingatia falsafa za malezi na makuzi ya mtoto zinazohimiza umuhimu wa miaka ya mwanzo ya mtoto kupata uangalizi na malezi bora kwani ni msingi wa maisha ya baadaye.